Ripoti mpya ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) imefichua takwimu za kutisha zinazoonesha jinsi mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la joto duniani yalivyosababisha mgogoro mkubwa wa chakula barani Afrika mwaka 2024. Ripoti hiyo iitwayo 'Hali ya Hewa Afrika 2024', iliyotolewa tarehe 13 Mei 2025, inaeleza kuwa mwaka jana ulikuwa wa pili kwa kuwa na joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa barani humo, hali iliyosababisha ukame na mafuriko yaliyoharibu mazao na kuathiri maisha ya mamilioni.
Kwa mujibu wa WMO, wastani wa joto la uso wa nchi kavu barani Afrika mwaka 2024 ulikuwa takriban nyuzi joto 0.86°C juu ya wastani wa muda mrefu (1991-2020). Kanda ya Kaskazini mwa Afrika ilirekodi ongezeko kubwa zaidi la joto, likifikia nyuzi joto 1.28°C juu ya wastani huo, ikithibitisha kuwa eneo hilo linapata ongezeko la joto kwa kasi zaidi barani Afrika.
Athari za hali hii mbaya ya hewa zilikuwa dhahiri kote barani:
Katika Kusini mwa Afrika, nchi za Malawi, Zambia, na Zimbabwe zilikumbwa na ukame mbaya zaidi katika kipindi cha takriban miaka 20. Mavuno ya nafaka kwa ujumla katika kanda hiyo yalipungua kwa asilimia 16 ikilinganishwa na wastani wa miaka mitano iliyopita. Hali ilikuwa mbaya zaidi nchini Zambia ambapo mavuno yaliporomoka kwa asilimia 43, na Zimbabwe kwa asilimia 50. Ukame huo pia ulisababisha kupungua kwa kina cha maji katika Bwawa la Kariba, ambalo ni bwawa kubwa zaidi la kutengenezwa na binadamu barani Afrika, na hivyo kupunguza uzalishaji wa umeme wa maji (hydropower). Hii ilisababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara na mivurugano ya kiuchumi.
Nayo Kaskazini mwa Afrika ilikabiliwa na ukame kwa mwaka wa tatu mfululizo, na kusababisha mavuno ya nafaka kuwa chini ya wastani. Nchini Morocco, uzalishaji wa nafaka mwaka jana unatarajiwa kupungua kwa asilimia 42 ikilinganishwa na wastani wa miaka mitano, huku Sudan ikitarajiwa kupungua kwa asilimia 35.
Hali haikuwa tofauti sana Afrika Mashariki. Kuanzia Machi hadi Mei 2024, mvua kubwa zisizo za kawaida zilinyesha na kusababisha mafuriko makubwa katika nchi za Kenya, Tanzania, na Burundi, na kuwaathiri zaidi ya watu 700,000. Aidha, kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huo huo, mvua zilikuwa chini ya wastani, na kuzua hofu kuhusu usalama wa chakula. Nchini Kenya pekee, mafuriko yalisababisha vifo vya zaidi ya mifugo 30,000 na kuharibu hekta 170,000 za mashamba. Hali hii nchini Tanzania ilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, makazi ya watu, na upotevu wa mazao, na kuwaacha wananchi wengi katika hali ngumu.
Kwa upande wa Afrika Magharibi na Kati, mafuriko yaliwaathiri zaidi ya watu milioni 4. Nchi zilizokuwa katika hali mbaya zaidi ni pamoja na Nigeria, Niger, Chad, Cameroon, na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ripoti ya WMO inachambua kuwa mabadiliko haya makali ya tabianchi yanazidisha baa la njaa barani Afrika na kuleta athari hasi katika nyanja zote za kijamii. Kutokana na athari hizi mbaya, sauti zinazidi kupazwa zikitaka ushirikiano wa kimataifa ili kusaidia nchi za Afrika kukabiliana na majanga haya ya tabianchi na kujenga uwezo wa kustahimili.
Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo, alisisitiza kuwa, "Baadhi ya nchi za Afrika zinakabiliwa na mafuriko yasiyo ya kawaida kutokana na mvua nyingi kupita kiasi, huku nyingine zikikabiliwa na ukame wa muda mrefu na uhaba wa maji." Aliongeza kuwa anatumai ripoti hiyo itachochea hatua za pamoja ili kukabiliana na athari hizi za mabadiliko ya tabianchi zinazozidi kuwa tata.