Serikali ya Japan inatarajia kuanza kusambaza mafuta ya mchanganyiko yanayochanganywa na bioethanol katika baadhi ya maeneo nchini humo kuanzia mwaka 2028. Hatua hii inalenga kupunguza kiwango cha gesi ya kaboni dioksidi inayozalishwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Gazeti la Yomiuri Shimbun limeripoti kuwa Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan inapanga kuanzisha kwa majaribio matumizi ya mafuta hayo, ambapo bioethanol itachanganywa na petroli kwa kiwango cha hadi asilimia 10.
Mpango huu unalenga kuharakisha jitihada za kupunguza utegemezi wa magari kwenye nishati inayochafua mazingira, kwani sekta ya usafirishaji inachangia takriban asilimia 20 ya uzalishaji wote wa gesi ya kaboni dioksidi nchini Japan. Bioethanol ni aina ya mafuta yanayotokana na vyanzo vya kibayolojia, mara nyingi huchukuliwa kutoka kwenye mimea kama vile mahindi au miwa. Huwa ni kimiminika chenye kileo na hutumika kama mafuta mbadala au kuchanganywa na petroli kutumika kwenye magari.
Awali, serikali ya Japan iliweka lengo la kuanza kusambaza mafuta hayo ya mchanganyiko yenye bioethanol kuanzia mwaka 2030. Hata hivyo, takriban asilimia 40 ya magari mapya yanayouzwa nchini Japan kwa sasa yana uwezo wa kutumia mafuta hayo ya mchanganyiko. Uamuzi wa kuanza awamu ya majaribio mapema, yaani kuanzia mwaka 2028 katika maeneo machache, unatokana na umuhimu wa kufanya tathmini ya kina kuhusu usalama, ubora na utendaji kazi wa mafuta hayo kabla ya kuanza kuyatumia kikamilifu kitaifa mwaka 2030.
Maeneo yatakayoanza kutumia mafuta haya ya majaribio yatakuwa yale yaliyo karibu na vituo vya kusafishia mafuta au maghala makubwa ya kuhifadhia mafuta. Maelezo zaidi kuhusu maeneo haya yanatarajiwa kutolewa katika nusu ya pili ya mwaka huu. Gazeti la Yomiuri Shimbun limeripoti kuwa serikali ya Japan imekuwa ikishirikiana kwa karibu na kampuni za kusafishia mafuta na watengenezaji wa magari ili kupata ridhio lao kabla ya kutekeleza mpango huu. Serikali imeahidi kutoa ruzuku kusaidia gharama za kufanya marekebisho kwenye vituo vya mafuta ili viweze kuhimili na kusambaza mafuta haya mapya.
Kwa siku za usoni, Japan ina mipango ya kufikia hatua ambapo magari yote mapya yanayotengenezwa kuanzia miaka ya mapema ya 2030s yataweza kutumia mafuta yenye mchanganyiko wa bioethanol kwa kiwango cha asilimia 20. Ifikapo mwaka 2040, serikali inalenga kuanza kusambaza rasmi mafuta yenye mchanganyiko wa asilimia 20 ya bioethanol. Kwa mujibu wa Yomiuri Shimbun, Japan inatarajia kuagiza bioethanol kutoka nchi kama Brazil na Marekani. Hata hivyo, changamoto kubwa itakuwa kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali hii kwa wingi na kwa bei nafuu.
Matumizi ya nishati mbadala kama bioethanol yanaongezeka duniani kote. Nchi kama Brazil na Uingereza tayari zimeweka sheria zinazotaka kuchanganywa kwa kiwango fulani cha bioethanol kwenye mafuta ya kawaida. Umoja wa Ulaya (EU) pia unahimiza matumizi ya bioethanol au nishati nyingine za kibayolojia kuchanganywa na petroli au dizeli ili kupunguza utoaji wa gesi chafuzi kutoka kwa injini za mwako wa ndani. Hata hivyo, kuna mijadala inayoendelea kuhusu faida halisi za bioethanol kwa mazingira. Baadhi ya wataalamu wa mazingira na mashirika ya kimataifa yanahoji ufanisi wa kupunguza kaboni kwa kuzingatia mchakato mzima wa uzalishaji wa bioethanol, huku wengine wakidai kuwa bioethanol inaweza hata kuwa na athari mbaya zaidi kwa mazingira kuliko petroli safi. Pamoja na changamoto na mijadala hii, Japan inaonekana kuazimia kutumia bioethanol kama njia mojawapo ya kufikia malengo yake ya mazingira.