Hali ya taharuki imetanda nchini Ufaransa baada ya vyama vikuu vya wafanyakazi kuitisha mgomo wa nchi nzima jana, Oktoba 2, kupinga vikali mipango ya serikali ya kubana matumizi. Mgomo huo umesababisha usumbufu mkubwa na kusababisha hata kivutio maarufu cha utalii duniani, Mnara wa Eiffel jijini Paris, kulazimika kufunga milango yake kwa wageni.
Maelfu ya wafanyakazi, wastaafu, na wanafunzi walimiminika kwenye mitaa ya zaidi ya miji 200 nchi nzima. Lengo lao ni moja: kuishinikiza serikali mpya ya Waziri Mkuu, Sébastien Lecornu, itupilie mbali rasimu ya bajeti iliyoachwa na mtangulizi wake, ambayo inaonekana kuumiza zaidi wananchi wa kipato cha chini na cha kati. Waandamanaji wanadai serikali iongeze kodi kwa matajiri badala ya kukata matumizi kwenye huduma muhimu za jamii.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imekadiria kuwa takriban watu 195,000 walishiriki maandamano hayo kote nchini, huku 24,000 wakiwa katika jiji la Paris pekee. Hii ni mara ya tatu kwa maandamano makubwa kufanyika ndani ya mwezi mmoja, jambo linaloonyesha kiwango kikubwa cha hasira ya wananchi hata kabla ya serikali mpya haijatangaza rasmi bajeti yake.
Akizungumza na kituo cha habari cha BFM TV, kiongozi wa chama cha wafanyakazi cha CGT, Sophie Binet, alisema, "Hii ni mara ya kwanza katika historia kuwa na migomo mitatu mikubwa ndani ya mwezi mmoja bila hata serikali kuwa na bajeti rasmi. Hii inadhihirisha kiwango cha hasira iliyopo kwenye jamii."
Ingawa mgomo huu umeonyesha nguvu ya umma, idadi ya walioshiriki imepungua ikilinganishwa na maandamano ya Septemba 18, ambapo zaidi ya watu nusu milioni walijitokeza. Licha ya hayo, huduma za usafiri ziliathirika kwa kiasi, huku baadhi ya safari za treni za mikoani zikisitishwa. Wakati Ufaransa ikisubiri kwa hamu kuona sura ya bajeti mpya, hali ya sintofahamu ya kisiasa na kijamii inaendelea kutawala nchi hiyo.