Hali ya taharuki na simanzi imegubika Jiji la Sydney nchini Australia, baada ya kile kilichotarajiwa kuwa sherehe za furaha na amani kugeuka kuwa "machinjio" ya kutisha. Katika tukio ambalo limeacha dunia ikiwa imeshika mdomo, watu 15 wamepoteza maisha kikatili baada ya kushambuliwa kwa risasi katika tamasha la sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah, lililofanyika katika fukwe maarufu za Bondi.
Serikali ya Australia, kupitia kwa Waziri Mkuu wake, Anthony Albanese, imethibitisha pasipo shaka kuwa shambulio hilo ni la kigaidi na lina uhusiano wa moja kwa moja na itikadi kali za kundi la Islamic State (IS).
Baba Amponza Mwana: Familia ya Kigaidi
Kinachoumiza zaidi na kuacha maswali mengi ni wasifu wa wahusika wa unyama huu. Imebainika kuwa waliotekeleza mauaji hayo ni Sajid Akram (50) na mwanaye wa kumzaa, Naveed Akram (24). Kitendo cha baba kushirikiana na mwanae katika kutekeleza ukatili wa kiwango hiki kimeelezwa na wachambuzi wa masuala ya kijamii kama "uovu uliopitiliza" na mmomonyoko wa maadili ya familia.
Akizungumza na kituo cha Taifa cha habari cha ABC, Waziri Mkuu Albanese alisema, "Uchunguzi wetu unaonyesha wazi kuwa hawa watu walisukumwa na chuki iliyopandikizwa na itikadi za ISIS. Kwa zaidi ya miaka kumi, itikadi hizi zimekuwa zikihubiri chuki ambayo leo imezaa maandalizi ya mauaji ya halaiki."
Mkuu wa Polisi wa Shirikisho la Australia, Kamanda Chrissy Barrett, aliongeza kuwa ushahidi wa awali unaonyesha kuwa wawili hao, baba na mwana, walifanya tukio hilo kama "timu ya maangamizi" iliyoathiriwa na mafundisho hayo potofu.
Safari ya Mindanao na Bendera za IS
Uchunguzi wa kina umeibua siri nzito kuhusu nyendo za magaidi hawa kabla ya tukio. Imebainika kuwa wawili hao walisafiri kuelekea nchini Ufilipino mwezi uliopita. Rekodi za uhamiaji zinaonesha kuwa Sajid (mwenye asili ya India) na Naveed (raia wa Australia), waliingia Ufilipino Novemba 1 na kurejea Sydney Novemba 28, zikiwa ni siku chache tu kabla ya kufanya mashambulizi.
Walipokuwa Ufilipino, walitembelea eneo la Kusini mwa kisiwa cha Mindanao, mkoa wa Davao del Sur. Eneo la Mindanao linafahamika kimataifa kama ngome ya makundi yenye misimamo mikali, ambapo mwaka 2017, wanamgambo wa IS walifanikiwa kuuteka mji wa Marawi na kusababisha vita vya miezi mitano vilivyogharimu maisha ya zaidi ya watu 1,100. Polisi wa Australia sasa wanachunguza nani walikutana naye huko "msituni" na kama huko ndiko walikopokea baraka za kufanya shambulio hili.
Katika gari walilotumia kufika eneo la tukio, polisi walikuta vitu vya kutisha: mabomu ya kutengeneza kienyeji (IEDs) na bendera mbili za ISIS zilizoshonwa kwa mkono, ishara tosha kuwa walidhamiria kuua watu wengi zaidi.
Naveed Alikuwa 'Kwenye Rada'
Inasikitisha kubaini kuwa kijana Naveed hakuwa mgeni kwa vyombo vya usalama. Mwaka 2019, aliwahi kuhojiwa na Shirika la Usalama la Australia (ASIO) kutokana na kuhusishwa na mpango wa kigaidi. Hata hivyo, wakati huo, licha ya watu wawili aliokuwa akishirikiana nao kufungwa jela, yeye hakuonekana kama tishio kubwa ("Primary Suspect"), jambo ambalo sasa linaonekana kama mwanya uliotumiwa vibaya.
Aidha, imebainika kuwa Naveed alikuwa mfuasi mkubwa wa mhubiri mwenye utata, Wissam Haddad, ambaye anafahamika kwa hotuba zake za chuki dhidi ya Wayahudi. Ijapokuwa Haddad hajawahi kushtakiwa kwa ugaidi, wafuasi wake wengi wameishia jela kwa makosa ya kigaidi, akiwemo mtu aliyedai kuwa "Kamanda wa IS Australia".
Kwa sasa, baba mtu, Sajid Akram, ameuawa katika majibizano ya risasi na polisi eneo la tukio, huku mtoto wake, Naveed, akiwa mahututi hospitalini chini ya ulinzi mkali wa polisi akisubiri mkono wa sheria.
Tukio hili ni ukumbusho mwingine kwa dunia, na hata Tanzania, kuwa vita dhidi ya ugaidi na itikadi kali bado inahitaji ushirikiano wa dhati kuanzia ngazi ya familia.