Dunia imefunikwa na wingu zito la simanzi na taharuki kubwa kufuatia tukio la kinyama lililotokea katika Jiji la Sydney nchini Australia, ambapo watu wa familia moja, Baba na Mwanawe, wamegeuka kuwa maadui wa uhai na kusababisha maafa makubwa. Eneo maarufu la kitalii la Bondi Beach, ambalo kwa kawaida hufurika watalii na kicheko, limegeuka kuwa uwanja wa damu baada ya watu hao kufanya shambulio la kutisha la kigaidi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizotolewa na Jeshi la Polisi la New South Wales leo tarehe 15, imethibitishwa pasipo shaka kuwa walioendesha mauaji hayo ya halaiki ni baba mwenye umri wa miaka 50 akishirikiana na kijana wake wa kiume mwenye umri wa miaka 24. Tukio hili la aina yake limewaacha wengi midomo wazi, ikizingatiwa kuwa uhalifu wa kutumia silaha nzito kiasi hicho nchini Australia si jambo la kawaida.
Siku ya Furaha Yageuka Karaha
Tukio hilo lilitokea jana jioni, majira ya saa 12:40 jioni, wakati mamia ya wananchi na watalii walipokuwa wamekusanyika kusherehekea sikukuu ya 'Hanukkah', ambayo ni sherehe muhimu ya kitamaduni na kiimani kwa jamii ya Wayahudi kuadhimisha kutakaswa kwa Hekalu la Pili.
Mashuhuda wanaeleza kuwa sherehe hizo zilizokuwa zikihudhuriwa na zaidi ya watu 1,000 katika eneo la Campbell Parade, ghafla ziliingia doa baada ya wanaume wawili waliovalia mavazi meusi, mfano wa makomando, kuanza kurusha risasi ovyo kwa muda wa dakika 10 mfululizo.
Vilio na Damu Isiyo na Hatia
Katika hali inayosikitisha, shambulio hilo limesababisha vifo vya watu 16, wakiwemo watoto wadogo wasio na hatia ambao walifika eneo hilo kufurahia sikukuu. Aidha, zaidi ya watu 40 wamejeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika hospitali mbalimbali jijini Sydney kwa ajili ya matibabu ya dharura, huku hali za baadhi yao zikielezwa kuwa mahututi.
Polisi walifanikiwa kumdhibiti baba mtu kwa kumpiga risasi na kumuua papo hapo eneo la tukio ili kuzuia madhara zaidi, huku mtoto wake akipata majeraha makubwa na sasa yuko chini ya ulinzi mkali hospitalini. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa baba huyo alikuwa anamiliki silaha hizo kisheria, akiwa na leseni halali ya bunduki zipatazo sita, jambo ambalo limezua mjadala mpya kuhusu sheria za umiliki wa silaha nchini humo.
Lengo la Kigaidi
Akizungumza na vyombo vya habari, ikiwemo Shirika la Habari la Reuters, afisa mwandamizi wa Polisi amemtajia mmoja wa washukiwa hao kwa jina la 'Naveed Akram' anayetokea Kusini Magharibi mwa Sydney, ingawa bado haijawekwa wazi kama jina hilo ni la baba au la mwanae.
Jeshi la Polisi limelihusisha tukio hilo moja kwa moja na ugaidi, likieleza kuwa halikuwa tukio la bahati mbaya bali mpango uliosukwa kulenga jamii ya Wayahudi. "Hili ni shambulio lililolenga jamii ya Wayahudi kwa makusudi kabisa," ilieleza taarifa ya polisi, huku wakihakikishia umma kuwa hakuna washukiwa wengine wanaotafutwa na kwamba hali ya usalama inadhibitiwa.
Tukio hili limetikisa hisia za watu kote duniani, huku viongozi mbalimbali wakilaani kitendo hicho cha kikatili kinachoenda kinyume na haki za binadamu na utu. Australia, nchi ambayo imekuwa ikisifika kwa utulivu wake, sasa inakabiliwa na mtihani mzito wa kuimarisha usalama na mshikamano wa kijamii dhidi ya chuki za kidini na rangi.