Washington D.C., Marekani – Wakati dunia ikiwa bado inaugulia maumivu ya kiuchumi na kibinadamu yatokanayo na vita vinavyoendelea sasa, Taasisi maarufu ya Kidiplomasia na Mahusiano ya Kigeni ya Marekani (Council on Foreign Relations - CFR), imetoa ripoti mpya inayochora picha ya kutisha kwa mwaka ujao, ikitabiri uwezekano mkubwa wa Marekani kujiingiza vitani moja kwa moja nchini Venezuela.
Ripoti hiyo, iliyopewa jina la 'Preventive Priorities Survey (PPS)', imeandaliwa na Kituo cha Kuzuia Migogoro (CPA) kilicho chini ya CFR, baada ya kukusanya maoni ya wataalamu wa usalama, maafisa wa serikali, na wanazuoni zaidi ya 620. Utabiri huu umeweka wazi kuwa mwaka 2026 unaweza kuwa mwaka wa "moto na baruti" katika pembe mbalimbali za dunia.
Marekani vs Venezuela: Moto wa Kuotea Mbali
Jambo lililoshitua wengi katika ripoti hii ni utabiri wa Marekani kupeleka majeshi yake nchini Venezuela. Wachambuzi hao wameeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Marekani kuanzisha operesheni za kijeshi kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya uhalifu na dawa za kulevya, jambo ambalo linaweza kubadilika na kuwa shambulizi la moja kwa moja dhidi ya serikali ya Rais Nicolás Maduro. Hatua kama hiyo inaweza kuliingiza bara la Amerika ya Kusini katika machafuko mapya na kuathiri soko la mafuta duniani, jambo ambalo linaweza kuumiza pia nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kupitia kupanda kwa bei ya nishati.
Mashariki ya Kati na Ulaya: Hakuna Dalili ya Amani
Ripoti hiyo imeendelea kubainisha kuwa, mgogoro wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina unatarajiwa kuwa mbaya zaidi. Eneo la Ukingo wa Magharibi (West Bank) linatajwa kuwa litashuhudia mapigano makali kutokana na ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiisraeli, huku vita vya Gaza vikitarajiwa kuibuka upya na kusababisha maafa makubwa ya kibinadamu.
Hali kadhalika, vita vya Urusi na Ukraine havionyeshi dalili ya kwisha. Wataalamu hao wameonya kuwa pande zote mbili zinatarajiwa kuzidisha mashambulizi kwenye miundombinu muhimu na makazi ya watu, jambo litakalozidi kuvuruga mnyororo wa usambazaji wa chakula na ngano duniani.
"Trump na Siasa za Ndani": Marekani Kuchafuka?\
Kitu cha kipekee katika ripoti ya mwaka huu ni angalizo kuhusu hali ya ndani ya Marekani yenyewe. Ripoti imetaja kuwa chini ya utawala wa pili wa Donald Trump, kuna hatari ya kuibuka kwa vurugu za kisiasa na machafuko ya ndani (civil unrest). Hii inatokana na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na uwezekano wa matumizi ya nguvu za kijeshi ndani ya nchi hiyo kudhibiti wapinzani au maandamano, jambo ambalo ni nadra kutokea katika taifa hilo linalojinasibu kama kiranja wa demokrasia.
Afrika na Asia: Sudan na Korea Kaskazini
Ingawa ripoti inasema migogoro ya Afrika inaweza isiathiri sana maslahi ya moja kwa moja ya Marekani, imeonya kuhusu kuendelea kwa umwagaji damu nchini Sudan, hali mbaya ya usalama Haiti, na mivutano ya uchaguzi nchini Sudan Kusini.
Kwa upande wa Asia, kitisho cha Korea Kaskazini kurejelea majaribio ya nyuklia kimetajwa kama "bomu linalosubiri kulipuka", likiwa na uwezekano wa kusababisha mzozo utakaohusisha mataifa makubwa (Great Powers). Pia, choko choko za China dhidi ya Taiwan na mashambulizi ya mtandaoni (Cyber attacks) yanayotumia akili mnemba (AI) ni mambo ya kuchungwa kwa jicho la karibu.
Ripoti imehitimisha kwa kusema kuwa, idadi ya migogoro ya silaha duniani kwa sasa imefikia kiwango cha juu zaidi tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. "Wakati utawala wa Trump ukijigamba kupata mafanikio, wataalamu wa usalama wanaona giza nene mbele," ilisema sehemu ya ripoti hiyo, ikisisitiza kuwa amani ya dunia ipo shakani zaidi kuliko wakati wowote ule.