Katika kile kinachoonekana kama "kamari ya mwisho" ya kujihami, serikali ya kijeshi ya Sudan, ambayo imekuwa ikipambana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, imeripotiwa kumuwekea mezani Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ofa ambayo ni ngumu kuikataa. Ripoti za kiintelijensia zilizochapishwa na gazeti la Wall Street Journal (WSJ) zinabainisha kuwa Sudan imependekeza kuikodishia Urusi bandari muhimu katika Bahari ya Shamu (Red Sea) kwa kipindi cha miaka 25 ili iweke kambi yake ya kijeshi.
Hatua hii, ikiwa itatimia, itabadilisha kabisa ramani ya nguvu za kijeshi duniani na kuipa Urusi "ufunguo" wa kuingia na kutoka Afrika na Mashariki ya Kati bila kizuizi, jambo ambalo limeibua hofu kubwa Washington na kwa washirika wa Magharibi.
"Nipe Silaha, Nikupe Ardhi na Dhahabu"
Mkataba huo uliopendekezwa mwezi Oktoba unaonesha sura halisi ya msemo wa wahenga, "Mkono mtupu haulambwi." Sudan, ambayo imelemewa na vita dhidi ya kikundi cha wanamgambo cha RSF (Rapid Support Forces), inahitaji silaha za kisasa haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa dili hilo:
- Urusi: Itaruhusiwa kujenga kituo cha kijeshi (Naval Base) kitakachokuwa na uwezo wa kuhifadhi askari hadi 300 na kupaki meli nne za kivita kwa wakati mmoja, zikiwemo zile zinazotumia nishati ya nyuklia (Nuclear-powered ships).
- Sudan: Itapokea mifumo mipya ya ulinzi wa anga (Anti-air systems) na silaha nzito kutoka Moscow ili kuwadhibiti waasi.
- Dhahabu: Urusi itapewa kipaumbele katika uchimbaji wa madini ya dhahabu nchini humo. Ikumbukwe Sudan ni mzalishaji wa tatu kwa ukubwa wa dhahabu barani Afrika.
Putin Apata "Dirisha" la Bahari ya Hindi
Kwa miaka mitano sasa, Kremlin imekuwa ikiiwinda fursa hii kama simba anayemvizia swala. Urusi imekuwa ikitafuta bandari ambayo haigandi (warm-water port) ili kurahisisha operesheni zake za majini.
Kambi hii itaiwezesha Urusi:
- Kudhibiti njia kuu ya biashara ya Mfereji wa Suez (Suez Canal), ambapo asilimia 12 ya biashara yote duniani hupita hapo. Hii ni njia muhimu pia kwa meli zinazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutokea Ulaya.
- Kuwa na uwezo wa kufanya operesheni za kijeshi katika Bahari ya Hindi na Bahari ya Mediterania kwa urahisi zaidi.
- Kurejesha heshima na ushawishi wake barani Afrika kama ilivyokuwa enzi za Usovieti.
Meja Jenerali Mstaafu wa Marekani, Mark Hicks, amekaririwa akisema: "Hili ni dili tamu kwa Putin. Kuwa na kambi Afrika kunampa heshima ya kimataifa na kutanua mabavu ya Urusi."
Marekani na China: Vita ya 'Kuitawala' Afrika
Wakati Moscow ikichekelea, Washington inahaha. Marekani imekuwa ikijitahidi kuzuia Urusi na China zisishikilie bandari muhimu za Afrika. Hofu kubwa ya Marekani ni kwamba, kukitokea vita au mtafaruku, Urusi inaweza kutumia kambi hiyo kufunga njia ya Bahari ya Shamu na kuzuia meli za mafuta na bidhaa kupita.
China, kwa upande wake, tayari ilishajijengea kambi yake ya kijeshi nchini Djibouti tangu mwaka 2017, nchi ambayo ipo jirani na Sudan katika Pembe ya Afrika. Kuingia kwa Urusi katika eneo hilo kunafanya ukanda wa Bahari ya Shamu kuwa "eneo la hatari" lililojaa majeshi ya mataifa makubwa yenye maslahi tofauti.
Kwa sasa, si serikali ya Sudan wala Ikulu ya Kremlin iliyotoa tamko rasmi, lakini dalili zinaonyesha kuwa "mzigo umeanza kufungwa." Kwa Tanzania na nchi za Afrika Mashariki, hii ni ishara ya kuongezeka kwa ushindani wa mataifa makubwa katika ukanda wetu, jambo linaloweza kuwa na faida au hasara kiusalama huko tuendako.