Ubalozi wa Marekani ulioko jijini Jerusalem, Israeli, umetangaza kurejelea shughuli zake za kawaida kuanzia leo, tarehe 25, kufuatia kupungua kwa hali ya wasiwasi na mivutano ya kijeshi iliyokuwepo kati ya Israeli na Iran. Hatua hii inakuja kama ishara ya afueni katika ukanda wa Mashariki ya Kati, ambao ulikuwa katika hofu ya kuzuka kwa vita kamili.
Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake rasmi, ubalozi huo ulieleza kuwa kutokana na kutuliza kwa hali ya mambo, Idara ya Ulinzi wa Raia ya Israeli imeondoa vizuizi vyote vya kiusalama vilivyokuwa vimewekwa awali. "Kufuatia uamuzi huu, Ubalozi wa Marekani utafunguliwa na utaendesha shughuli zake kama kawaida," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ubalozi huo ulikuwa umesitisha huduma zake muhimu na kuwataka wafanyakazi wake pamoja na familia zao kuchukua tahadhari za hali ya juu kufuatia mashambulizi ya kulipizana visasi kati ya Israeli na Iran yaliyotikisa eneo hilo. Mvutano huo ulizua hofu ya kuzuka kwa mzozo mpana zaidi, na kusababisha nchi nyingi kutoa tahadhari kwa raia wake.
Kurejea kwa shughuli za ubalozi kunamaanisha kuwa huduma zote muhimu kwa raia, ikiwemo sehemu ya huduma za konseli inayoshughulikia utoaji wa pasipoti na viza, zitaanza kufanya kazi tena. Aidha, ushauri wa kuwaondoa wafanyakazi wa serikali ya Marekani na familia zao kutoka nchini humo umeondolewa rasmi.
Kufunguliwa tena kwa ofisi hizi muhimu za kidiplomasia ni ishara tosha ya kupungua kwa hatari ya haraka ya kijeshi, ingawa wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasisitiza kuwa chanzo cha msingi cha mzozo kati ya mataifa hayo hasimu bado kipo. Jamii ya kimataifa inaendelea kufuatilia kwa karibu, ikitumai kuwa hali ya utulivu itaendelea kudumu katika ukanda huo wenye changamoto nyingi za kiusalama.