Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza masikitiko yake makubwa na kulaani vikali matukio ya utekaji wa raia wawili katika mikoa ya Dar es Salaam na Kigoma, huku kikitilia shaka namna Jeshi la Polisi linavyoshughulikia matukio hayo. Chama hicho kimeonya kuwa vitendo hivi vinahatarisha usalama wa wananchi na vinaashiria ama udhaifu mkubwa wa vyombo vya dola au uwezekano wa kushiriki kwa baadhi ya maafisa wa usalama katika matukio hayo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa, Februari 28, 2025, Method Damian Kumdyamka (45) alitekwa nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam, na watu wanane waliokuwa na silaha na gari aina ya Prado. Familia yake iliripoti tukio hilo katika vituo vyote vya Polisi jijini Dar es Salaam na kufanya jitihada mbalimbali za kumtafuta, lakini hadi sasa hajapatikana. Pamoja na hali hiyo, Jeshi la Polisi limeonekana kutokuchukua hatua za haraka wala kutoa taarifa yoyote ya kina kuhusu uchunguzi wa tukio hilo.
Tukio jingine lilitokea Februari 10, 2025, ambapo Manase Daniel (40), maarufu kama ‘White’, alitekwa mchana kweupe akiwa katika duka lake la vipuri eneo la Senga, Kigoma Ujiji. Watekaji, waliokuwa na silaha, walimfunga pingu na kuondoka naye bila upinzani wowote. Ndugu zake waliripoti tukio hilo kwa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Wilaya na RTO, lakini hadi sasa hakuna taarifa yoyote rasmi kuhusu alipo. Manase, ambaye ni tegemeo la familia yake, ana mke, watoto sita, na baba yake mgonjwa aliyekuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji.
ACT Wazalendo imeeleza kuwa ukimya wa Jeshi la Polisi unazidi kuzua hofu miongoni mwa wananchi. Ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwa mbinu zilizotumika katika matukio hayo, kama vile matumizi ya silaha na pingu, zinafanana na mbinu za kiusalama, jambo linaloongeza mashaka kuhusu uwezekano wa kuhusika kwa baadhi ya maafisa wa usalama. Chama hicho kimetaka Serikali kueleza ikiwa watekaji ni watu wa kawaida au kuna mkono wa dola katika matukio haya.
Kutokana na hali hii, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani kupitia ACT Wazalendo, Dahlia Majid Hassan, ameitaka Serikali na vyombo vya usalama kuchukua hatua za dharura kuhakikisha haki inatendeka na usalama wa raia unarejeshwa. Chama hicho kimependekeza hatua zifuatazo zichukuliwe mara moja:
- Jeshi la Polisi litoke hadharani kueleza walipo wananchi waliotekwa na hatua zinazochukuliwa katika uchunguzi wa matukio haya.
- Uchunguzi huru na wa haraka ufanyike ili kubaini wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria.
- Serikali ihakikishe usalama wa raia na kusitisha mara moja mwenendo wa utekaji wa watu bila hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
ACT Wazalendo imeeleza kuwa Watanzania hawatakubali kuishi kwa hofu huku vyombo vya dola vikishindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda wananchi. Chama hicho kimetoa wito kwa Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya usalama na kuhakikisha kuwa matukio ya utekaji hayageuki kuwa hali ya kawaida nchini.