Katika kile kinachoashiria kuanza kazi kwa kishindo na kasi ya ‘4G’, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, ameanza majukumu yake kwa kutoa dira mpya kwa jeshi la uhifadhi nchini. Akifanya ziara yake ya kwanza ya kikazi katika Makao Makuu ya Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) tangu alipokabidhiwa kijiti hicho, Dk. Kijaji amesisitiza kuwa bunduki na sare za jeshi hilo hazipaswi kuwa tiketi ya kuwanyanyasa wananchi, bali ziwe nyenzo ya kuleta amani na maelewano.
Dk. Kijaji ameweka wazi kuwa falsafa mpya ya wizara hiyo ni “Uhifadhi wa Kibinadamu”, akitaka kuona askari wa wanyamapori wakiongozwa na utu, ukarimu, na uzalendo uliotukuka wanapokabiliana na changamoto za kila siku, ikiwemo migogoro ya mara kwa mara kati ya binadamu na wanyama wakali na waharibifu.
Vitendea Kazi vya Kisasa: Drones na Magari Ili kuendana na kasi ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya kidunia katika kupambana na ujangili, Dk. Kijaji hakufika mikono mitupu. Katika ziara hiyo, amekabidhi shehena ya vitendea kazi vitakavyorahisisha operesheni za TAWA katika mapori ya akiba na maeneo tengefu.
“Leo nimefika hapa TAWA kuwapa nguvu ya kazi. Tunakabidhi magari manne mapya, pikipiki 33 kwa ajili ya doria za vichochoroni, bajaji, na muhimu zaidi, tumeleta ndege nyuki (drones) kwa ajili ya ulinzi wa anga. Hii ni ishara kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kulinda rasilimali zetu kwa gharama yoyote,” alisisitiza Dk. Kijaji.
Matumizi ya ‘drones’ katika uhifadhi ni hatua kubwa kwa Tanzania, kwani inasaidia kufuatilia mienendo ya wanyama na majangili katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika kwa gari au miguu, hivyo kuongeza ufanisi wa kiintelijensia.
TAWA na Diplomasia ya Uhifadhi Waziri Kijaji alikumbusha kuwa TAWA ni taasisi inayoishi katikati ya jamii. Alibainisha kuwa mafanikio ya utalii hayategemei tu uzuri wa mbuga, bali jinsi wananchi wanavyoshirikishwa na kunufaika na rasilimali hizo.
“Ninyi ni sura ya serikali huko porini na vijijini. Askari wa uhifadhi lazima awe rafiki wa raia wema na adui wa wahalifu. Onyesheni utu mnaposhughulikia kero za wananchi wanaovamiwa na wanyama, kwani ukarimu wenu ndio utakaofanya wananchi wawe walinzi wa kwanza wa wanyama hawa,” aliongeza.
Tanzania: Ghala la Wanyama Duniani Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hassan Abbasi, alitoa takwimu ambazo zinaifanya Tanzania kuwa "Giant" wa uhifadhi barani Afrika. Dk. Abbasi alibainisha kuwa ongezeko la watumishi katika sekta hiyo miaka minne iliyopita limezaa matunda ya kuongezeka kwa idadi ya wanyamapori, jambo linaloipa nchi heshima kimataifa.
“Tanzania inabeba dhamana kubwa duniani. Tunasimamia uhifadhi wa rasilimali wanyama adimu na wengi. Takwimu zetu zinaonyesha tuna simba zaidi ya 17,000, nyati 225,000, tembo 60,000 na chui 24,000. Huu ni utajiri ambao mataifa mengi yanausikia kwenye bomba tu,” alifafanua Dk. Abbasi.
Idadi hii ya simba na tembo inaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache duniani zilizofanikiwa kuzuia kutoweka kwa wanyama hao walio katika hatari, na hivyo kuendelea kuwavutia watalii maelfu kwa maelfu kila mwaka kuja kushuhudia “The Big Five”.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Hamad Chande, alihitimisha kwa kuahidi ushirikiano dhabiti (teamwork) kati ya viongozi wa kisiasa na watendaji wa TAWA ili kuhakikisha sekta ya utalii inazidi kuliingizia taifa fedha za kigeni na kutoa ajira kwa vijana.