Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ametoa agizo kwa Wizara ya Kilimo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu umiliki wa ardhi inayoshikiliwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises Ltd katika wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya. Lengo la uchunguzi huo ni kubaini iwapo kampuni hiyo imeshindwa kuiendeleza ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria na kama kuna haja ya kurejesha ardhi hiyo serikalini kwa matumizi mengine yanayowanufaisha wananchi.
Wananchi wa Tukuyu, Rungwe, wamekuwa wakilalamika kuwa kampuni hiyo inamiliki mashamba makubwa ya chai ambayo yameachwa bila uzalishaji kwa muda mrefu. Hali hii imesababisha ardhi hiyo kugeuka mapori, ambayo yanavutia wanyama waharibifu na kuwanyima wakazi maeneo ya kulima.
Akizungumza na wananchi wakati wa ziara yake mkoani Mbeya, Wasira alisema kuwa CCM inaagiza serikali kufuatilia suala hilo kwa kina na kuhakikisha kuwa sheria za umiliki wa ardhi zinafuatwa. "Sheria ya ardhi inasema kuwa ukipatiwa ardhi, lazima uitumie kwa uzalishaji. Mashamba haya ya chai yakiacha kuzalisha, viwanda vya chai haviwezi kufanya kazi, na matokeo yake ni kudidimia kwa uchumi wa wananchi," alieleza Wasira.
Wasira alifafanua kuwa Tanzania haina mfumo wa umiliki wa ardhi wa milele (Free Hold), bali ina mfumo wa Lease Hold, ambapo ardhi hutolewa kwa masharti maalum ya uzalishaji. "Ukiacha mashamba yako yakiwa mapori, unavunja mkataba wa umiliki. Tunaiambia serikali kuwa kama Mohammed Enterprises imeshindwa, basi mashamba yarudi serikalini na yagawiwe kwa matumizi mengine," alisisitiza.
Aliongeza kuwa Rais wa Tanzania ana mamlaka ya kutwaa ardhi isiyotumika kwa maendeleo ya wananchi, na hivyo suala hilo linapaswa kushughulikiwa haraka ili wakazi wa Rungwe waweze kunufaika na ardhi hiyo.
Mbali na suala la ardhi, Wasira pia alizungumzia changamoto zinazowakabili wakulima wa chai na kahawa, hususan suala la kutolipwa kwa wakati. "Kuna mgogoro kati ya ushirika na wanunuzi wa kahawa. Waziri wa Kilimo amewaita Dodoma ili kuhakikisha suala hili linashughulikiwa na wakulima wanalipwa haraka," alisema. Aliongeza kuwa kampuni ya GDM, ambayo inanunua chai, haijalipa wakulima kwa miezi miwili na inadaiwa shilingi milioni 664. "Tunawapa wiki mbili wawe wamewalipa wakulima. Wasipofanya hivyo, tutaiomba serikali kuwanyima leseni ya biashara, kwa sababu hii ni dhuluma, na CCM hatuwezi kuvumilia dhuluma," alisema kwa msisitizo.
Wasira pia alizungumzia changamoto ya bei duni ya zao la parachichi wilayani Rungwe, ambayo imekuwa ikiwakumba wakulima wa eneo hilo. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalulenge, alieleza kuwa ubora wa parachichi kutoka Rungwe umekuwa changamoto katika soko la kimataifa, kwani matunda mengi hushambuliwa na fangasi tangu hatua ya maua, jambo linalosababisha kuoza haraka baada ya kuvunwa. "Tunalishughulikia suala hili kwa kushirikiana na Waziri wa Kilimo ili kuhakikisha wakulima wa parachichi wananufaika na mazao yao," alisema Mwalulenge.
Katika muendelezo wa ziara yake mkoani Mbeya, Wasira alitembelea wilaya ya Kyela na pia alikutana na mjane wa mwanzilishi wa TANU na CCM, marehemu Mzee John Mwakangale, kabla ya kuzungumza na wananchi wa Tukuyu, wilayani Rungwe. Ziara yake imelenga kuimarisha chama na kushughulikia kero zinazowakabili wananchi, hasa wakulima, ambao ni nguzo kuu ya uchumi wa Tanzania.