Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonyesha kuwa vijana wanajumuisha sehemu kubwa ya Watanzania, ikiwa ni asilimia 34.5 ya watu wote nchini. Hata hivyo, asilimia 21.7 ya vijana hao wanafanya kazi ambazo hazihitaji ujuzi maalum. Kutokana na changamoto hii, serikali ya Tanzania imeendelea kuwekeza kwa vijana kwa kuwapatia fursa mbalimbali za kiuchumi. Hizi ni pamoja na mikopo yenye riba nafuu ya asilimia nne inayotolewa na halmashauri za wilaya, pamoja na mikopo mingine yenye masharti nafuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pamoja na juhudi hizi, tatizo kubwa limekuwa uelewa mdogo wa vijana kuhusu fursa hizi, hali ambayo inawazuia kuzitumia kikamilifu na kuboresha maisha yao. Ili kukabiliana na changamoto hii na kuwasaidia vijana kuchangamkia fursa zilizopo, Taasisi ya Mulika Tanzania imeanzisha mpango maalum wa kuwawezesha kiuchumi vijana katika wilaya nne za Mkoa wa Dodoma. Mpango huu unahusisha kutoa mafunzo ya biashara, usimamizi wa fedha, na mbinu za kufikia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana.
Lengo kuu la mradi huu ni kuchangia katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan kwa kuwawezesha vijana kupitia ujasiriamali na fursa za ajira, ili kupunguza kiwango cha umasikini miongoni mwao. Ingawa kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa, vijana bado wanakabiliwa na changamoto nyingi, hasa katika kupata huduma bora za afya, elimu bora, na fursa za kiuchumi ambazo zinaweza kuwainua.
Akizungumza katika mafunzo yaliyofanyika kwa vijana wa Wilaya ya Chamwino, Ofisa Biashara wa wilaya hiyo, Grace Nkalalwe, alieleza kuwa kuna fursa nyingi za biashara ambazo vijana wanaweza kuzitumia kujikwamua kiuchumi. Alitolea mfano kilimo cha zabibu, ambacho kina soko kubwa katika eneo hilo, pamoja na fursa za mikopo zinazotolewa na halmashauri ya wilaya. Aliwahimiza vijana kutambua fursa zilizopo katika mazingira yao ili waweze kuanzisha biashara, hata kwa mtaji mdogo. "Unapotaka kuanzisha biashara, ni muhimu sana kwanza kufanya utafiti wa soko ili kuhakikisha kuwa bidhaa au huduma unayotoa itakuwa na faida," alishauri Nkalalwe.
Naye Ofisa Mikopo wa Halmashauri ya Chamwino, Mary Muhoza, alifafanua kuwa serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa kila halmashauri inatenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. Kati ya fedha hizo, asilimia nne zimetengwa kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana, na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu. Bi. Muhoza alieleza kuwa vijana wanapaswa kuunda vikundi vya watu wasiopungua watano, kuwa na wazo la biashara linaloeleweka, kuandaa katiba ya kikundi, na kusajili vikundi vyao katika mfumo rasmi kabla ya kuweza kuomba mikopo hiyo.
Ofisa Maendeleo wa Kata ya Buigiri, Veronica Baluwa, alisisitiza kuwa ni muhimu kwa vijana kuwa na mradi wa pamoja ambao wamekubaliana kabla ya kuomba mkopo. "Mradi huo ndio mtakaoutumia kuombea mkopo kupitia mfumo wa 'Wezesha Portal'," alifafanua Bi. Baluwa.
Baadhi ya vijana waliohudhuria mafunzo hayo walitoa ushuhuda jinsi mafunzo hayo yamewapa matumaini mapya ya kiuchumi. Yusta Awea (22), ambaye aliacha shule akiwa kidato cha pili kutokana na matatizo ya kifedha, alisema amehamasika sana kukuza biashara ya chakula anayofanya na mama yake kwa kutumia fursa za mikopo zinazopatikana. "Tumeshaanza kuunda vikundi na tuko katika hatua za kuandaa katiba ili tuweze kuomba mkopo," alisema Awea, akiongeza kuwa elimu ya mara kwa mara inaweza kuwasaidia vijana wengi ambao hukata tamaa kutokana na changamoto za mchakato wa kupata mikopo.
Ilumbo Fwejeje, ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Vijana Wajibika cha Buigiri, aliongeza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia sana kutambua fursa mbalimbali zilizopo na kujifunza jinsi ya kujiandaa kwa ajili ya kuomba mikopo. Fwejeje, ambaye ni fundi cherehani, alisema wameunda kikundi ambacho kinalenga kuanzisha biashara ya vifaa vya ushonaji na ufugaji wa nguruwe. "Tulishapeleka katiba yetu lakini tuliambiwa kuna marekebisho tunapaswa kufanya, hivyo tuko katika hatua za kurekebisha ili tuweze kupata mkopo," alieleza.
Kwa upande wake, Magreth Chalo, ambaye anajishughulisha na ufugaji wa bata na nguruwe, alisema kabla ya mafunzo hayo hakuwa anafahamu kuwa kuna mikopo inayotolewa na serikali kwa ajili ya vijana. Kupitia elimu waliyopewa na Taasisi ya Mulika Tanzania, yeye na wenzake walielekezwa jinsi ya kuunda vikundi na kuandaa na kuwasilisha andiko la biashara kwa ofisa maendeleo wa kata.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mulika Tanzania, Hussein Melele, alisema kuwa mradi huu unalenga kuwapa vijana wa makundi maalum fursa sawa za kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi, huku wakizingatia usawa wa kijinsia. "Kupitia mafunzo haya, vijana wa Dodoma wanaweza kuelewa fursa zilizopo katika wilaya za Bahi, Chamwino, Kondoa na Dodoma Mjini. Wanajifunza namna ya kubuni na kuendeleza mawazo ya biashara kwa kuzingatia mahitaji ya soko," alieleza Melele. Aliongeza kuwa mafunzo hayo pia yanawapa vijana uelewa kuhusu usimamizi wa fedha, matumizi sahihi ya mikopo, na huduma za kibenki ili waweze kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kukuza uchumi wao.
Inatarajiwa kuwa kwa kuendelea kuwapatia vijana maarifa na ujuzi muhimu, wataweza kuwa na mwamko mpya wa kiuchumi na kutumia vyema fursa zinazotolewa na serikali na taasisi mbalimbali, na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi wa familia zao na taifa kwa ujumla.