Ilala Yatoa Bilioni 18 za Mikopo, DC Mpogolo Aonya Wajanja, Aahidi Elimu

economy | Tue Jul 08 2025


Ilala Yatoa Bilioni 18 za Mikopo, DC Mpogolo Aonya Wajanja, Aahidi Elimu

Serikali katika Wilaya ya Ilala imezindua rasmi mpango wa utoaji mikopo ya asilimia kumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiweka mezani bajeti ya kihistoria ya Shilingi bilioni 18.3. Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo, ametangaza vita dhidi ya maombi yasiyo na uhalisia na kuahidi kushuka chini kutoa elimu ili fedha hizo ziwafikie walengwa sahihi.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, DC Mpogolo alisema bajeti hiyo kubwa imewezekana kutokana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, chini ya Mkurugenzi Elihuruma Mabelya, kuongeza makusanyo ya mapato maradufu kutoka Shilingi bilioni 61 hadi bilioni 130 kwa mwaka.


Licha ya fedha kuwepo, Mpogolo alieleza changamoto kubwa inayowakabili ni ubora wa maombi kutoka kwa vikundi. Alisema tayari vikundi 945 vimeomba mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 50, lakini vingi vina mapungufu.


"Unakuta mtu ana mradi wa kupika chipsi lakini anaomba mkopo wa Shilingi milioni 60. Mwingine ana genge la kuuza samaki lakini anaomba mkopo wa milioni 300. Wengine wanadai biashara zao ni za mtandaoni lakini hawana anuani halisi. Huu si usahihi na unakwamisha wengi kupata mikopo," alisema Mpogolo.


Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Mpogolo alitangaza mkakati wa pande mbili. Kwanza, ofisi yake itashuka hadi ngazi za mitaa kutoa mafunzo kwa vitendo kuhusu namna ya kuandaa maombi sahihi na kujaza fomu kidijitali. Pili, alitangaza ushirikiano na benki za CRDB na NMB katika kutoa na kusimamia mikopo hiyo ili kuongeza uwazi na ufanisi.


Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika Halmashauri ya Jiji, Rehema Sanga, alisema jukwaa lake liko tayari kushirikiana na serikali kuhakikisha mafanikio. Alisema wataanzisha mpango wa ushauri na ufuatiliaji ujulikanao kama "Mama wa Nguvu" na kusaidia vikundi kuandaa mipango ya biashara inayokubalika na benki, kwa lengo la kufikia kiwango cha urejeshaji cha zaidi ya asilimia 95.


Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika akiwemo Mama Godi, muuza samaki, wameishukuru serikali kwa kutimiza ahadi yake, wakisema mikopo hiyo itawasaidia kukuza mitaji yao na kuboresha maisha ya familia zao.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.