Uamuzi wa Serikali wa kuhamisha Stendi ya Mabasi ya Ubungo kwenda Mbezi Luis mwaka 2020 uliwapagawisha wengi, na baadhi ya wananchi walidhani kuwa huo ulikuwa mwisho wa uhai wa kiuchumi wa eneo hilo maarufu. Hofu ilienea kuwa wajasiriamali wadogo, mama lishe na wauza magazeti wangekosa soko lao, na kwamba mitandao ya biashara iliyojengwa kwa miongo kadhaa ingekufa. Lakini leo, Agosti 1, 2025, historia imeandikwa upya na mawazo hayo yakafutika kabisa baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) jijini Dar es Salaam.
Hatua hii ya kishindo ya kugeuza Ubungo kuwa kituo cha biashara chenye hadhi ya kikanda na kimataifa ni ushahidi tosha wa maono ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Badala ya kuona changamoto kama mwisho wa safari, Rais Samia ameigeuza kuwa fursa kubwa ya maendeleo, inayotoa ajira kwa maelfu ya Watanzania na kuimarisha uchumi wa nchi. Kwa mujibu wa vyanzo vya Serikali, uamuzi wa kuhamisha stendi haukulenga tu kupunguza msongamano wa magari, bali ulikuwa sehemu ya mpango kabambe wa kufungua sura mpya ya kibiashara, sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26.
EACLC si jengo la kawaida, bali ni kitovu cha kimkakati kinacholenga kuunganisha nchi za Afrika Mashariki kiuchumi, kurahisisha biashara, usambazaji wa bidhaa na huduma, huku ikitumia teknolojia ya kisasa kuongeza tija. Kituo hiki kinatumika kama nguzo muhimu ya utekelezaji wa Itifaki ya Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA).
Kutokana na mradi huu, manufaa ya moja kwa moja yameanza kuonekana. Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imethibitisha kuwa tayari kituo hicho kimeaanza kutoa zaidi ya ajira 3,000 za moja kwa moja, huku kukiwa na matarajio ya kufikia ajira zaidi ya 10,000 zisizo za moja kwa moja ifikapo mwaka 2026. Kwa upande wa mapato ya Serikali, EACLC inakadiriwa kuchangia zaidi ya Shilingi bilioni 50 kwa mwaka kupitia kodi mbalimbali kama vile VAT, kodi ya mapato, na tozo za manispaa.
Kwa mujibu wa ripoti ya World Bank ya mwaka 2023, gharama za usafirishaji bidhaa barani Afrika ni kubwa sana, ikifikia kati ya asilimia 18-22 ya thamani ya bidhaa. EACLC inatarajiwa kupunguza gharama hizi kwa asilimia 5 hadi 8 kwa kuanzisha mifumo ya kisasa na ya haraka. Hili litaifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara, na tayari wawekezaji zaidi ya 300 kutoka nchi jirani kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC wameonyesha nia ya kuwekeza.
Rais Samia, wakati akizindua kituo hiki, alisisitiza kuwa EACLC haipingani na Soko la Kariakoo bali inaongeza wigo wa biashara na kutoa fursa ya kujifunza matumizi ya teknolojia ili kuongeza thamani ya bidhaa. Kwa mtazamo mpana, ujenzi wa EACLC ni sehemu ya maono ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji wa kikanda, lengo ambalo sasa linaonekana kuzaa matunda. Eneo la Ubungo, lililokuwa likihofiwa kufa kiuchumi, sasa linang'aa na miundombinu ya kisasa, huduma za kibenki, bima na teknolojia ya hali ya juu, likionyesha jinsi maono mazuri yanavyoweza kugeuza changamoto kuwa fursa.