Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imefanikiwa kukusanya kiasi kikubwa cha dhahabu safi cha tani 6.84, chenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 682.66 (sawa na takribani Shilingi za Tanzania trilioni 1.7). Mafanikio haya yameiweka Tanzania miongoni mwa nchi 10 bora barani Afrika zinazohifadhi dhahabu iliyosafishwa kama sehemu ya akiba yake ya fedha za kigeni.
Mpango huu wa serikali wa kununua dhahabu ulianza kuratibiwa tangu Julai 2024, huku utekelezaji wake rasmi ukianza Oktoba mwaka jana. Lengo kuu ni kuimarisha akiba ya fedha za kigeni ya taifa kupitia rasilimali hii muhimu. Taarifa hizi zimetolewa leo na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akifunga mafunzo ya kukuza ujuzi kwa wachimbaji wadogo, yaliyotolewa na Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu.
Dkt. Kiruswa alibainisha kuwa Sheria ya Madini ya mwaka 2019, kupitia Kifungu cha 59, Sura ya 123, inaelekeza wazi kwamba yeyote anayetaka kuuza dhahabu nje ya nchi, lazima asilimia 20 ya dhahabu hiyo iuzwe kwa Benki Kuu ya Tanzania. Kanuni hii inahakikisha kuwa nchi inanufaika ipasavyo na rasilimali zake.
"Sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi na kuchangia pakubwa katika pato la taifa, kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023/24 hadi kufikia asilimia 10.1 mwaka huu," alisema Dkt. Kiruswa. Aliongeza kuwa sekta hii pia imechangia kiasi kikubwa cha Shilingi Trilioni 1.07 katika mfuko mkuu wa serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25, jambo linaloonyesha mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi.
Kuhusu mafunzo hayo, Dkt. Kiruswa alieleza kuwa yamelenga kuwapatia wachimbaji wadogo ujuzi wa nadharia na vitendo, ambao utasaidia kuboresha uzalishaji wa madini kuanzia hatua za utafiti, uchimbaji salama na ufanisi, uchenjuaji, usalama na afya mahali pa kazi, hadi matumizi sahihi ya vilipuzi.
"Hizi zote ni hatua za kuunga mkono serikali katika kuleta mabadiliko chanya kwa wachimbaji wadogo. Tunatambua kwamba tuna fursa kubwa ya kujitajirisha kupitia shughuli ya madini, na sekta hii ni sekta tarajiwa katika kutengeneza mabilionea nchini Tanzania," alisisitiza Naibu Waziri.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bi. Alana Nchimbi, amefafanua kuwa mafunzo hayo ya wiki mbili yamewanufaisha jumla ya wachimbaji wadogo 479. Bi. Nchimbi alifafanua kuwa mpango wa serikali wa kukuza ujuzi ulianza mwaka 2016, na hadi Juni mwaka huu, serikali imetumia jumla ya Shilingi Bilioni 111 (takribani Dola za Kimarekani milioni 42.4) na kuwanufaisha wanufaika 157,909.
Alana Nchimbi alieleza kuwa programu hii inatoa mafunzo katika maeneo manne makuu: mafunzo ya uanagenzi (apprenticeship), uzoefu kazini (on-the-job training), mafunzo ya urasimishaji ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu (recognition of prior learning), na mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi. Mafunzo haya yamewajengea wachimbaji uelewa mpana kuhusu kanuni za usalama kazini, mbinu bora za uchimbaji endelevu, mikakati ya kutafuta masoko, na namna ya kushirikiana na taasisi za kifedha kupata mitaji.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Geita, Bw. Titus Kabuo, alishukuru serikali kwa mafunzo hayo. Alisema kuwa wachimbaji mara nyingi hulazimika kuchimba chini sana, na bila ujuzi sahihi wa kuchimba na kulinda mashimo, ni rahisi kupoteza maisha. Alibainisha kuwa kupitia mafunzo hayo, wamejifunza namna ya kutunza kumbukumbu za kazi, kufanya kazi kwa ufanisi, na kujipatia kipato. Kabuo alipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa iliyoifanya katika sekta ya madini, ikiwemo kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo na kupunguza tozo zilizokuwa zikikwamisha maendeleo yao.