Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), imefanya tangazo rasmi kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya EXPO 2025 yatakayofanyika Osaka, Japan. Maonyesho haya yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 12 Aprili hadi 13 Oktoba, 2025, na yanatarajiwa kuvutia zaidi ya watu milioni 28.2 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Suleiman Jafo, alieleza kuwa kauli mbiu ya maonyesho hayo ni “Kuwezesha Jamii kwa Maisha Endelevu”. Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha ushirikishwaji wa jamii katika maendeleo kwa kutumia ubunifu na teknolojia ili kuchochea ukuaji wa uchumi katika mataifa mbalimbali.
“Maonyesho haya ni fursa muhimu sana kwa Tanzania kujitangaza kimataifa katika sekta mbalimbali muhimu kama vile viwanda, biashara, uwekezaji, utalii, na teknolojia. Kupitia ushiriki wetu katika EXPO 2025, tunatarajia kupata matokeo chanya katika kuimarisha uelewa wetu wa taarifa za biashara. Hii itaiwezesha Tanzania kutambua fursa mpya za masoko katika ngazi ya kimataifa,” alifafanua Waziri Jafo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Angelina Ngalula, alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika maonyesho hayo. Alisema kuwa sekta binafsi itajikita hasa katika kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini Tanzania, kuvutia wawekezaji kutoka nje, kukuza sekta ya utalii, kutafuta washirika wa kibiashara, na kujifunza mbinu mpya na za kisasa za uendeshaji wa biashara.
“Teknolojia na ubunifu vitakuwa msingi mkuu katika ushiriki wa Tanzania kwenye EXPO 2025. Tutatumia fursa hii kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika sekta muhimu kama vile afya, nishati, madini, utalii, kilimo, uchumi wa buluu, sanaa na utamaduni,” alibainisha Bi. Ngalula.
Zaidi ya hayo, Bi. Ngalula alitangaza kuwa kwa kushirikiana na TanTrade, Tanzania imeandaa Kongamano Kubwa la Biashara, Uwekezaji na Utalii ambalo litafanyika tarehe 26 Mei, 2025. Kongamano hili ni sehemu muhimu ya maandalizi kuelekea EXPO 2025 na litatoa fursa kwa wadau mbalimbali wa sekta kukutana na makampuni makubwa yenye nia ya kuwekeza au kushirikiana kibiashara na Tanzania.
“Kongamano hili litahusisha utiaji saini wa mikataba ya ushirikiano kati ya taasisi kutoka Tanzania na Japan, kubadilishana uzoefu katika biashara, pamoja na jitihada za kuvutia mitaji kwa ajili ya biashara na kuhamasisha watalii kuja kutembelea nchini Tanzania,” aliongeza Bi. Ngalula.
Tanzania ni moja ya nchi ambazo zitashiriki kwa nguvu katika Maonyesho ya EXPO 2025 Osaka. Kupitia jukwaa hili, Tanzania inatarajia kuinua hadhi yake katika masuala ya uchumi na diplomasia kimataifa, kujenga uhusiano imara na mataifa mengine, na kuvutia fursa mbalimbali za maendeleo.