Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Seleman Jafo, ametoa wito kwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kujitangaza kimataifa ili kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali. Waziri Jafo alisisitiza kuwa chuo hicho kina uwezo mkubwa wa kuwa kitovu cha elimu ya biashara kwa wanafunzi wa kimataifa, kutokana na ubora wa elimu inayotolewa ambayo inakidhi viwango vya kimataifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa Bodi ya Uongozi ya CBE, Dk. Jafo alieleza kuwa ni muhimu kwa CBE kutumia fursa hii ili kuongeza wigo wake na kuchangia katika kuimarisha uchumi wa nchi kupitia elimu. Aliongeza kuwa badala ya kutegemea wanafunzi wa ndani pekee, chuo kinaweza kuwa na ushawishi mkubwa katika soko la elimu ya kimataifa.
Sambamba na hilo, Waziri Jafo aliwahimiza vijana nchini kushirikiana na kampuni za uzalishaji ili kutumia fursa za soko la Afrika kupitia mpango wa African Growth and Opportunity Act (AGOA). Mpango huu unatoa nafasi ya bidhaa takriban 6,500 kutoka Afrika kuingia katika soko la Marekani bila kulipa ushuru. Alisema kuwa hii ni fursa ya kipekee ambayo Tanzania inapaswa kuitumia kikamilifu ili kukuza biashara na uchumi.
“Mpango wa AGOA unatoa fursa kubwa kwa bidhaa za Tanzania kufika Marekani, lakini bado hatujaitumia ipasavyo. Tunapaswa kufanya bidii zaidi ili kuchangamkia soko hili na kuhakikisha Watanzania wananufaika,” alisema Waziri Jafo. Aliongeza kuwa ni jukumu la CBE kuandaa vijana wenye ujuzi wa kutosha ili waweze kushiriki katika biashara za kitaifa na kimataifa kwa kuwawezesha maarifa ya ushindani wa kibiashara.
Dk. Jafo alibainisha kuwa Tanzania imefungua milango yake kwa masoko ya kimataifa, hivyo kuna haja ya kuwa na vijana wenye maarifa sahihi ili kushirikiana na wazalishaji wa ndani kuuza bidhaa za Tanzania kimataifa. Alitaja masoko ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kama fursa nyingine kubwa kwa vijana wa Tanzania.
Aidha, alitaka CBE kuandaa programu za mafunzo ya muda mfupi kwa wafanyabiashara ili kuwajengea uwezo zaidi wa kushiriki katika biashara ya kimataifa. Alipendekeza mafunzo kuhusu uongozi, namna ya kuandika barua za kuomba kazi, na jinsi ya kufanya usaili, akieleza kuwa mafunzo ya wiki moja au mbili yanaweza kuwasaidia watu wengi sana.
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, alieleza mafanikio ya bodi iliyomaliza muda wake (2021-2024), ikiwemo kuandaa dira ya miaka 50 ya chuo (2025-2075). Alisema bodi hiyo iliongeza udahili wa wanafunzi kutoka 10,034 mwaka 2021 hadi 22,263 mwaka 2024, na kupanua programu za masomo kutoka astashahada hadi shahada za uzamili. Pia, ilianzisha shahada za umahiri mtandaoni na shahada ya uzamivu katika biashara ya informatiki.
Profesa Lwoga alieleza kuwa bodi hiyo iliboresha miundombinu kwa kuanza ujenzi wa jengo la ghorofa 10 la metrolojia, linalogharimu Shilingi za Kitanzania bilioni 22.4, ambapo awamu ya kwanza itakamilika Juni 2025.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdalah, alipongeza mchango wa CBE katika kufanya tafiti za kuboresha sekta ya biashara. Mwenyekiti wa Bodi mpya, Profesa Zacharia Mganilwa, alisema kuwa kuwa na wataalamu wenye ujuzi ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania, na CBE ina jukumu la kuhakikisha vijana wanapata maarifa na uwezo wa kuendesha biashara zenye ushindani wa kimataifa.