Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yanayotarajiwa kufanyika Machi 8, 2025, kwa kaulimbiu inayosisitiza "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji," Wizara ya Nishati imeeleza fahari yake kwa hatua kubwa iliyopigwa katika kulinda haki, usawa, na kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini kupitia upatikanaji wa uhakika wa umeme na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza kuhusu maandalizi kuelekea siku hii muhimu, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, alieleza kuwa wizara yake imefanya kazi kubwa katika kuhakikisha wanawake wanapata umeme na nishati safi ya kupikia, hatua ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha yao na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
"Tayari tumefanikiwa kupeleka umeme katika zaidi ya vitongoji 33,000 kote nchini. Sambamba na hilo, kupitia programu mbalimbali za wizara, tumeweza kugawa mitungi ya gesi takribani 402,000 kwa wanawake, majiko banifu zaidi ya 200,000, pamoja na majiko ya umeme, yote kwa lengo la kuwasaidia wanawake kupata nishati bora na salama ya kupikia," alieleza Mhe. Kapinga. Aliongeza kuwa hatua hii imepunguza kwa kiasi kikubwa muda ambao wanawake walikuwa wanautumia kutafuta kuni, na hivyo kuwawezesha kuwa na muda zaidi wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Mhe. Kapinga alibainisha kuwa uwekezaji huu mkubwa katika sekta ya nishati unalenga moja kwa moja kuboresha ustawi wa wanawake na kuwapa nguvu ya kushiriki kikamilifu zaidi katika shughuli za maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Alieleza kuwa nishati safi si tu inalinda afya zao kutokana na moshi hatari, bali pia inawapa fursa ya kuwa na muda zaidi wa kujishughulisha na shughuli za kiuchumi na elimu.
Mbali na mafanikio katika sekta ya nishati, Mhe. Kapinga alipongeza pia juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuboresha sekta za elimu na afya, akitolea mfano Sera ya Elimu Bila Malipo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike wanaojiunga na shule. Aidha, alieleza kuwa maboresho yanayoendelea kufanywa katika huduma za afya yamewasaidia wanawake kupata matibabu bora na kwa wakati, hali ambayo inawawezesha kuendelea na shughuli zao za uzalishaji bila vikwazo vikubwa vya kiafya.
Pia, Mhe. Kapinga alimpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kutambuliwa kwake kimataifa kupitia Tuzo ya Goalkeeper. Tuzo hii ilitolewa kutokana na mchango wake mkubwa katika kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kwa asilimia 80, pamoja na mafanikio katika kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa kila vizazi 1,000. Alisema kuwa kutambuliwa huku ni ushahidi wa dhamira ya serikali katika kuboresha maisha ya wanawake na watoto nchini.
Kwa ujumla, Wizara ya Nishati imesisitiza kuwa itaendelea kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuleta mabadiliko chanya kwa wanawake nchini, kuhakikisha kuwa masuala ya haki, usawa, na maendeleo yao yanapewa kipaumbele katika sera na mikakati yote ya wizara.