Rais Samia Suluhu Hassan ameweka wazi vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu nchini, ambao wanaghushi risiti za mashine za EFDs na stempu za kodi kwenye bidhaa za vinywaji ili kukwepa kulipa kodi stahiki. Rais ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuchukua hatua za haraka na kali dhidi ya wizi huu unaokosesha serikali mapato muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa walipakodi bora kwa mwaka wa fedha 2023/2024, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Rais Samia alieleza kuwa vitendo hivi vya wizi ni dhuluma kwa Watanzania wote na vinakwamisha juhudi za serikali katika kuleta maendeleo. “Nina taarifa za kughushi stempu za ushuru wa bidhaa za vinywaji. TRA iligundua sakata hili mapema, na kama wasingefanya hivyo, serikali ingepoteza zaidi ya shilingi bilioni 200 za Kitanzania,” alisema Rais Samia kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa baadhi ya kampuni pia zinakwepa kulipa kodi kwa kutumia mbinu ya kughushi risiti za mashine za EFDs. Rais aliitaka TRA kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wale wote wanaohusika na vitendo hivi vya uhalifu. “Nawataka TRA kusimama imara dhidi ya uhalifu huu. Wakati tunatoa tuzo kwa walipakodi bora, ni muhimu pia kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka sheria na kutulazimisha kutumia nguvu kudai kodi,” alisisitiza Rais Samia.
Rais Samia alisisitiza umuhimu wa uadilifu kwa watumishi wote wa TRA na kuwataka kuchukua hatua za haraka dhidi ya wale wanaojihusisha na rushwa na ukwepaji wa kodi. Alisema kuwa mazingira ya rushwa ni adui wa haki na maendeleo ya nchi. “Watumishi wote wanaojihusisha na vitendo hivi wanapaswa kuchukuliwa hatua mara moja,” alionya.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa hiari na uaminifu ili kusaidia kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa. Serikali, kwa upande wake, inaendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha mchakato huo.
Rais Samia alielezea dhamira ya serikali ya kupunguza utegemezi wa kibajeti kwa kukuza mapato ya ndani. Alisema kuwa lengo ni kuwa na mfumo wa kodi unaotabirika, usio na usumbufu kwa walipakodi, huku ukichagiza ukuaji wa uchumi. “Tunataka mfumo wa kodi ambao unarahisisha ukuaji wa biashara, unaongeza mapato, na kujenga taifa lenye kujiamini,” alisema.
Alikumbusha kuwa mwaka jana, serikali iliunda Tume ya Maboresho ya Kodi ili kufanya tathmini ya mfumo wa kodi na kuleta mapendekezo ya maboresho. Mpango huo unalenga kuimarisha mazingira ya biashara, kukuza ajira, na kuongeza mapato ya serikali.
Rais Samia pia alitangaza kuwa kuanzia mwaka ujao, tuzo za walipakodi bora zitakuwa chini ya Ofisi ya Rais badala ya TRA, ili kuongeza hadhi na kuwapa motisha wafanyabiashara wanaolipa kodi kwa uzalendo. Alisisitiza umuhimu wa kuhimiza sekta isiyo rasmi kuingia kwenye sekta rasmi ili kuongeza wigo wa walipakodi na kuimarisha mapato ya taifa. “Ni lazima tuweke mikakati itakayofanya sekta isiyo rasmi kuhitimu na kuwa sehemu ya sekta rasmi,” alisisitiza.
Katika tukio hilo, TRA ilitangaza Benki ya NMB, Tanzania Breweries Company (TBL), na CRDB Bank kuwa washindi bora wa ulipaji kodi kwa hiari, huku Kampuni ya Bakhresa ikishinda tuzo kwa upande wa sekta binafsi.
Rais Samia alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka wafanyabiashara kuwa mabalozi wema katika jamii zao, akisisitiza kuwa ulipaji kodi ni uzalendo na hatua muhimu kwa ustawi wa taifa.