Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka wazi mabadiliko makubwa katika sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/26, ambapo sasa wafanyabiashara wadogo maarufu kama "wamachinga" wataingia kwenye mfumo mpya wa usajili na ulipaji kodi, huku waendesha bodaboda wakiondolewa kodi rasmi. Mabadiliko haya ni sehemu ya marekebisho ya takriban sheria 11 za kodi nchini.
Akifafanua utaratibu huo mpya mjini Singida, Afisa Forodha Mkuu wa TRA, Zephaniah Mange, alisema jukumu la kuwasajili wamachinga sasa limehamishiwa kutoka TRA kwenda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. "Kabla ya Julai 1, mwaka huu, machinga alikuwa akisajiliwa na TRA na kulipa Sh. 20,000. Katika utaratibu mpya, wizara ndiyo itawasajili na kupendekeza kiwango cha kodi watakacholipa. Hata hivyo, sasa kila mmoja atalazimika kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN)," alisema Mange. Alifafanua kuwa mfumo huu unawalenga wafanyabiashara wenye mauzo yasiyozidi Shilingi milioni 4 kwa mwaka.
Habari njema zaidi ni kwa waendesha bodaboda, ambao kwa mujibu wa Mange, wameondolewa rasmi kwenye mfumo wa kodi uliokuwa umewaweka katika mwaka wa fedha uliopita. Hatua hii inaonekana kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kuwapunguzia mzigo wananchi waliojiajiri katika sekta hii muhimu ya usafirishaji.
Kwa upande wake, Ofisa Msimamizi wa Kodi wa TRA, Jamal Ngarawa, alieleza kuwa lengo la marekebisho haya mapana ya sheria za kodi ni kulinda viwanda vya ndani, kupanua wigo wa walipakodi, na muhimu zaidi, kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje, hasa katika kufadhili sekta ya afya. Alitolea mfano ongezeko dogo la tozo za viwanja vya ndege, akisema mapato hayo yanakwenda moja kwa moja kwenye Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote na mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI.
"Lengo letu siyo kutoza faini, bali kuwa marafiki wa walipakodi. Tunatoa elimu hii ili wananchi walipe kodi kwa hiari na kuepuka adhabu," alisema Ngarawa, akisisitiza kuwa utii wa sheria huongezeka pale elimu inapotolewa. Miongoni mwa sheria zilizoguswa na marekebisho haya ni pamoja na Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sheria ya Kodi ya Mapato, na Sheria ya Michezo ya Kubahatisha.