Zama za halmashauri nchini kutegemea kikamilifu bajeti ya serikali kuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo huenda zikafika ukingoni, kufuatia wito mzito uliotolewa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC). Kituo hicho kimezitaka mamlaka za serikali za mitaa (halmashauri) kubuni na kuibua miradi ya kimkakati itakayotekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka sekta binafsi.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mratibu wa Miradi ya Ubia katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wa PPPC, Msoleni Dakawa, alisema mtindo huu utaziwezesha halmashauri kujitegemea kimapato na kuharakisha maendeleo badala ya kusubiri fedha za serikali ambazo mara nyingi hazitoshelezi.
"Halmashauri nyingi zina fursa kubwa lakini zinashindwa kuzitumia. Badala ya kuiweka miradi kwenye bajeti na kusubiri, ni bora kuiandaa na kuitangaza kwa sekta binafsi. Hii itaziongezea mapato ya kujiendesha," alisema Dakawa.
Ili kufanikisha hili, Dakawa alizishauri halmashauri kuchukua hatua tatu muhimu: kwanza, kutenga fedha kidogo kwa ajili ya kuandaa nyaraka za kitaalamu za miradi ili iwe rahisi kuitangaza. Pili, kwa taasisi zinazomiliki ardhi, ni muhimu zihakikishe zinapata hatimiliki za ardhi hizo ili kuondoa vikwazo kwa wawekezaji. Tatu, kubuni miradi inayovutia na yenye faida kwa mwekezaji na jamii kwa ujumla.
Alitaja baadhi ya miradi inayoweza kutekelezwa kwa mtindo huu kuwa ni pamoja na ujenzi wa masoko ya kisasa, vituo vya mabasi na malori, vituo vya afya, shule na vyuo binafsi, maeneo ya starehe, na hata viwanja vya michezo (sports arena).
Kwa mujibu wa sheria, miradi midogo ya ubia katika ngazi ya halmashauri ina ukomo wa uwekezaji wa hadi Shilingi bilioni 50, huku miradi mikubwa ikiwa ni ile inayozidi thamani hiyo.
Kituo cha PPPC kinaendelea kutoa elimu kwa viongozi wa umma na wananchi kwenye banda lao katika viwanja vya Sabasaba, kikiwasihi kutumia fursa hiyo kujifunza namna ya kushiriki katika mtindo huu wa ubia unaolenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi kutoka ngazi ya chini.