Katika kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kuwa 'ng'ombe wa maziwa' kwa uchumi wa Taifa na kufikia malengo makubwa yaliyowekwa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, amefanya ziara ya kistratejia katika Makao Makuu ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo mazito yanayolenga kuleta mapinduzi ya kifikra na kiutendaji.
Akiwa katika ziara hiyo iliyofanyika Novemba 26, 2025, Dk. Kijaji ameweka wazi kuwa zama za kufanya kazi kwa mazoea zimepita. Amesisitiza kuwa Bodi hiyo inabeba dhamana kubwa ya kuhakikisha Tanzania inafikia lengo la kuvutia watalii milioni nane (8,000,000) ifikapo mwaka 2030. Lengo hili si namba tu, bali ni mkakati wa kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa vijana kupitia mnyororo wa thamani wa utalii.
Ubunifu na Bidhaa Mpya Sokoni Waziri Kijaji amebainisha kuwa Tanzania imebarikiwa vivutio vingi ambavyo bado ni "lulu iliyofichwa". Ameitaka TTB kuumiza kichwa na kuja na bidhaa mpya za utalii badala ya kutegemea vivutio vilivyozoeleka pekee (kama Mlima Kilimanjaro na Serengeti).
"Ni bidhaa chache tu ndizo zimepelekwa sokoni na kugeuzwa fedha. Tunataka vivutio zaidi vitangazwe na kutambulika kimataifa. Lazima tuwe wabunifu wa kuhakikisha mgeni anayekuja nchini haridhiki na kuondoka tu, bali anatamani kurudi tena na anakuwa balozi wa kuwaleta wengine," alisisitiza Dk. Kijaji.
Sayansi ya Masoko na Utafiti Akigusia suala la ushindani wa kibiashara duniani, Waziri huyo msomi ameiagiza TTB kuwekeza nguvu kwenye utafiti wa kina (Market Intelligence). Ameelekeza kuwa bodi hiyo inapaswa kushirikiana na taasisi nyingine kubaini mahitaji mahususi ya watalii kulingana na asili yao.
"Lazima tujue mteja wetu anataka nini. Mtalii wa China ana matakwa tofauti na Mtalii wa Marekani au Ulaya. Tunapaswa kujua lugha zao, misimu wanayopenda kusafiri na aina ya vyakula au uzoefu wanaoutafuta. Bila data sahihi, tutakuwa tunapiga gizani," alieleza.
Urithi wa 'Royal Tour' na Soko la Asia Dk. Kijaji hakusita kupongeza jitihada zilizofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya The Royal Tour na kipindi maarufu cha Amazing Tanzania. Alibainisha kuwa programu hizi zimefungua milango mipya, hususan katika soko la China ambako mwitikio umekuwa mkubwa.
Hata hivyo, kama kiongozi mwenye maono, ameshauri kuwa mafanikio hayo yasibaki China pekee. "Hii kasi ya Amazing Tanzania tuipeleke na kwa majirani zao. Masoko ya Asia yana nguvu kubwa ya kiuchumi na idadi kubwa ya watu wanaopenda kusafiri. Tutanue wigo huko," alishauri.
AFCON 2027: Fursa ya Dhahabu Kuelekea michuano mikubwa ya soka barani Afrika (AFCON 2027) ambayo Tanzania ni mwenyeji mwenza, Waziri Kijaji ameitaka TTB kuacha kulala usingizi. Ameagiza kuandaliwa kwa mkakati maalum (Master Plan) wa kutumia mashindano hayo kutangaza utalii.
"AFCON 2027 si mpira tu, ni biashara na utalii. Wageni watakaokuja kushangilia timu zao ni lazima wapate fursa ya kuona uzuri wa Tanzania. Bodi lazima iwe kiungo kati ya sekta binafsi na wageni hawa ili kuhakikisha kila fursa inatumika kikamilifu," alihitimisha Dk. Kijaji.
Ziara hii ya Dk. Kijaji imewasha taa nyekundu kwa watendaji wa sekta ya utalii, ikiashiria kuwa serikali inatarajia matokeo makubwa na ya haraka katika kukuza idadi ya watalii na mapato ya nchi.