Mnamo Juni 2020, serikali ilipitisha uamuzi wa kubadili mfumo wa ukusanyaji mapato ya utalii, ikiondoa jukumu hilo kutoka kwa mamlaka za hifadhi (TANAPA na NCAA) na kulikabidhi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Wakati huo, baadhi ya wabunge, wakiongozwa na Zitto Kabwe, walitoa angalizo zito: "Serikali ina mwenendo usioridhisha wa kutoa fedha za maendeleo, uamuzi huu ni hatari kwa uhifadhi." Miaka mitano baadaye, ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha kuwa angalizo hilo halikuwa la kupuuza.
Uamuzi huo, uliolenga kuongeza ufanisi, sasa unaonekana kuwa kilema kinachokwamisha sekta inayochangia asilimia 17.2 ya Pato la Taifa. Licha ya TRA kukusanya mamia ya mabilioni kutoka kwenye vyanzo vya utalii, fedha za maendeleo hazirudi ipasavyo kwenye hifadhi hizo, na kusababisha miradi muhimu kukwama na miundombinu kuzorota.
Uhalisia Kwenye Takwimu za CAG
Ripoti za CAG zimefichua ukweli mchungu. Kwa mfano, ripoti ya mwaka wa fedha 2023/24 inaonyesha kuwa wakati TRA ilikusanya Shilingi bilioni 637.6 kwa niaba ya TANAPA na NCAA, mgao wa fedha za maendeleo kwa mamlaka hizo ulikuwa wa kusikitisha. NCAA, iliyoidhinishiwa na Bunge Shilingi bilioni 28.61 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, haikupokea hata shilingi moja—iliambulia sifuri. Kwa upande wa TANAPA, kati ya Shilingi bilioni 23.03 zilizoidhinishwa kwa ajili ya miundombinu, ni Shilingi bilioni 1.06 pekee ndizo zilizotolewa.
"Kutolewa fedha chini ya bajeti kunachangia kutotekelezwa kwa miradi... hali hii ikiendelea, itasababisha kuzorota kwa miundombinu, itaathiri ukuaji wa utalii na hatimaye kupunguza mapato kwa serikali," anaonya CAG Charles Kichere katika ripoti yake.
Sauti Kutoka Mbugani
Matokeo ya ufinyu huu wa bajeti yanaonekana moja kwa moja kwenye hifadhi. Afisa mmoja mwandamizi wa TANAPA alikiri kuwa wamepitia kipindi kigumu, ambapo miradi 15 yenye thamani ya Shilingi bilioni 14.12 imechelewa kukamilika kwa miezi 10 hadi 33. Shughuli muhimu kama kudhibiti mimea vamizi na ukarabati wa barabara zimekwama.
"TANAPA ilipanga kutengeneza barabara za urefu wa kilomita 6,712, lakini imeweza kutengeneza kilomita 4,022 tu kutokana na ukosefu wa fedha," inasema ripoti ya CAG.
Chacha Nyandongo, mwongoza watalii mwenye uzoefu wa miaka 22, anasema hali ya barabara ni mbaya. "Fikiria barabara zina mashimo, mvua ikinyesha magari yanakwama na wakati mwingine yanapinduka na wageni. Mtalii akipata ajali hifadhini, usitegemee ataisema vyema Tanzania akirejea kwao," anaonya Chacha.
Suluhu Mpya na Mashaka Yake
Kutokana na shinikizo, serikali, kupitia kwa Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, imetangaza marekebisho ya sheria. Sasa, mamlaka hizo zitaruhusiwa kubaki na asilimia 51 ya mapato yao. Hata hivyo, sheria hiyo mpya ina sharti: lazima waombe kibali kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali kabla ya kutumia fedha hizo.
Hali hii imezua mashaka mapya. Kamati ya Bunge ya Bajeti na wadau kama Chacha Nyandongo wanahoji kama asilimia 51 inatosha, na kama sharti la kuomba kibali halitaendeleza urasimu na ucheleweshaji uliokuwepo awali. Ni kama alivyosema Mbunge Priscus Tarimo bungeni, "Ng'ombe anayekamuliwa hachinjwi, bali analishwa vizuri." Swali linabaki: Je, marekebisho haya mapya yanatosha kumlinda na kumlilia "ng'ombe" huyu anayelipatia taifa mabilioni?