Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, amewataka viongozi wa taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake zinazohusika na masuala ya uhifadhi kuhakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kulinda maeneo ya hifadhi kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Balozi Dkt. Chana alitoa agizo hilo leo, Machi 29, 2025, alipokuwa akizungumza na Uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Arusha National Park) wakati wa ziara yake ya kikazi. Katika ziara hiyo, alikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita 16, ambayo inagharimu shilingi za Kitanzania milioni 417.8. Barabara hii inaunganisha kata ya Ngarenanyuki na Usa River, katika Wilaya ya Arumeru, Mkoani Arusha.
"Katika jitihada zetu za kupambana na ujangili na uvamizi katika maeneo yetu ya hifadhi, umefika wakati muafaka wa kutumia teknolojia za kisasa kulinda rasilimali zetu. Tunapaswa kutumia vifaa kama vile ndege zisizo na rubani (drones), darubini za kisasa, kamera za CCTV, na teknolojia nyinginezo," alisisitiza Balozi Dkt. Chana.
Aidha, Balozi Dkt. Chana aliipongeza menejimenti ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa kazi nzuri wanayoifanya na kwa kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 6 katika mwaka wa fedha 2019/2020 hadi kufikia shilingi bilioni 9 katika mwaka wa fedha 2023/2024. Pia alishukuru kwa ongezeko la idadi ya watalii kutoka 57,697 hadi 81,761 katika kipindi hicho hicho.
"Nawapongeza sana, na Mheshimiwa Rais anafurahishwa sana na shughuli za utalii zinavyoendelea na ukusanyaji mzuri wa mapato," alisema Balozi Dkt. Chana.
Katika hatua nyingine, Balozi Dkt. Chana alikazia umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti ya kuzuia na kupunguza matukio ya wananchi kujeruhiwa na wanyamapori wakali wanaotoka katika hifadhi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Bwana Musa Kuji, aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na kuhakikisha kuwa wanaendelea kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo na kuongeza mapato zaidi katika siku zijazo.
Balozi Dkt. Chana yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ambapo, pamoja na mambo mengine, atatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Ziara hii inalenga kuhakikisha kuwa sera na mikakati ya wizara inatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya taifa.