Kilimo cha Kahawa Kilimanjaro Hatarini, Sheria Maalum ya Ulinzi Yadaiwa Haraka

economy | Wed Sep 10 2025


Kilimo cha Kahawa Kilimanjaro Hatarini, Sheria Maalum ya Ulinzi Yadaiwa Haraka

Sauti za wasiwasi zimetawala katika uzinduzi wa msimu wa sita wa Tamasha la Kahawa mjini Moshi, huku wakulima na wadau muhimu wa zao hilo wakielezea hofu yao juu ya mustakabali wa kahawa mkoani Kilimanjaro. Kiini cha hoja yao ni kitendo cha baadhi ya wananchi kung'oa na kukata ovyo mimea ya kahawa, ambayo ni utambulisho na urithi wa kihistoria wa mkoa huo, ili kupisha ujenzi wa makazi ya kisasa.


Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake, Bwana Julius Mollel alitoa ombi zito kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu. Alisisitiza umuhimu wa serikali, kupitia Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), kuandaa na kuwasilisha Bungeni muswada wa sheria utakaotoa ulinzi wa kisheria kwa zao la kahawa. Alieleza kuwa, nchi nyingi zinazoongoza kwa uzalishaji wa kahawa duniani zina sheria thabiti zinazodhibiti ukataji wa mibuni.


"Tunakuomba Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, wazo hili lifikishwe serikalini. Lazima tuwe na sheria inayomlazimu mtu anayetaka kung'oa kahawa kupata kibali maalumu kutoka kwa wataalamu, ambao watajiridhisha na sababu zake," alisema Mollel. Alionya kuwa bila kinga hiyo ya kisheria, ajenda ya kuinua kahawa itakufa na Mkoa wa Kilimanjaro utapoteza alama yake kuu ya utambulisho.


Kauli hiyo iliungwa mkono kwa hisia kali na Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu, ambaye hakuchelea kuonyesha masikitiko yake. Alikemea vikali tabia inayoibuka katika maeneo ya milimani ambapo mashamba mazima ya kahawa yanaangamizwa ili kujenga nyumba za kifahari. Babu alitahadharisha kuwa mwelekeo huo ni hatari na unatishia kurudisha nyuma jitihada za kuirejesha Tanzania kwenye ramani ya dunia ya wazalishaji bora wa kahawa. "Chapa yetu sisi ni kahawa. Sasa kama kila mtu anakata mibuni ajenge nyumba, tunakoelekea siko. Ni lazima tupambane kuzuia uharibifu huu," alisisitiza Babu.


Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo, alifafanua malengo ya tamasha hilo, akisema ni jukwaa la kuhamasisha unywaji wa kahawa nchini na kuitangaza kimataifa. Alisema tamasha hilo linaonyesha fursa pana zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa kahawa, kuanzia kwenye utalii wa kimazingira (eco-tourism), ambapo wageni hupata fursa ya kujionea mchakato mzima kutoka shambani hadi kikombeni. Aliongeza kuwa sekta hii inatengeneza ajira nyingi kwa vijana katika Nyanja za ugani, uchumaji, ukaangaji, na usafirishaji.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.