Zaidi ya Shilingi bilioni 1.3 zimeanza kutolewa rasmi kama fidia kwa wananchi wa maeneo ya Mkata, Handeni na Kilindi, waliopisha utekelezaji wa Mradi muhimu wa Gridi Imara unaolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini. Zoezi hili linaashiria hatua muhimu katika kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa huku haki na maslahi ya wananchi vikipewa kipaumbele cha juu.
Akizindua rasmi ulipaji wa fidia hizo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, alisema kuwa kitendo cha serikali kutoa fedha hizo ni uthibitisho wa jinsi inavyothamini mchango na uwekezaji wa wananchi wake katika maendeleo. Alitoa wito mzito kwa wananchi hao, akiwataka sasa wageuke kuwa walinzi namba moja wa miundombinu hiyo ya umeme itakayonufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
"Serikali imetimiza wajibu wake kwa kulipa fidia hii inayojali utu wenu. Sasa ni jukumu letu sote kutunza miundombinu hii. Tukiruhusu iharibiwe, hasara itakuwa ni yetu sote," alisisitiza Nyamwese.
Kwa mujibu wa Meneja wa mradi huo, Mhandisi Jafari Mpina, kukamilika kwa Gridi Imara katika eneo la Handeni kutafungua fursa nyingi za kiuchumi. Alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika utachochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati, kuvutia viwanda vidogo na hivyo kuongeza ajira kwa wananchi.
Ili kuhakikisha usalama na uwazi, Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Handeni, Carlos, alithibitisha kuwa malipo yote yanafanyika moja kwa moja kupitia akaunti za benki za wanufaika. Hii inaondoa hatari ya upotevu wa fedha na kuwapa walengwa uhakika wa kupata stahiki zao kikamilifu. Wananchi waliopokea fidia zao hawakusita kuishukuru serikali, wakisema fedha hizo zitawapa fursa ya kuboresha maisha yao na kuwekeza katika shughuli nyingine za kiuchumi.