Mkoa wa Lindi unatarajiwa kuwa kituo muhimu cha uchimbaji wa madini nchini Tanzania kutokana na kugundulika kuwa na akiba kubwa ya zaidi ya aina kumi za madini mbalimbali, ikiwa ni pamoja na madini ya kimkakati kama vile grafiti (kinywe) na nikeli.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emmanuel Shija, amesema kuwa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) mwaka 2024 kwa kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drone) umeonesha kuwepo kwa wingi wa madini ya kimkakati ya grafiti katika eneo la Ruangwa ndani ya Mkoa wa Lindi.
Aina nyingine za madini ambayo yamegunduliwa kuwepo kwa wingi ni pamoja na madini yenye asili ya chuma kama vile nikeli, dhahabu, shaba, manganese, pamoja na madini ya viwandani kama jasi, chokaa, chuma, na chumvi.
Mhandisi Shija alieleza zaidi kuwa Mkoa wa Lindi tayari unazalisha kwa kiasi kikubwa madini ya viwandani ya jasi, ambayo hutumika sana katika viwanda vya saruji na kutengeneza bidhaa za 'gypsum board' kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na nchi jirani.
"Mkoa wa Lindi kwa sasa tunauelezea kama 'The Future Mineral Hub of Tanzania' (kitovu cha uchimbaji madini cha baadaye cha Tanzania). Licha ya kutokuwa na miradi mingi mikubwa kwa sasa, matarajio yetu ni kwamba ndani ya miaka michache ijayo tutakuwa na miradi mikubwa ya madini ndani ya mkoa wetu," alisema Mhandisi Shija na kuongeza, "Hii inatokana na ukweli kwamba kuna upatikanaji wa madini mbalimbali kwa kiwango kikubwa."
Alisema kuwa kwa sasa kuna mradi wa uchimbaji wa kati wa Lindi Jumbo ambao umeanza kuzalisha madini ya grafiti yenye ubora wa hali ya juu kwa ajili ya matumizi katika betri na vifaa vya kielektroniki.
"Hali ya uzalishaji ni nzuri katika makusanyo yetu. Tuna aina kuu tatu za madini ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa mapato. Nikeli inaongoza kwa kuchangia asilimia 35 ya makusanyo, ikifuatiwa na madini ya dhahabu ambayo yanachangia asilimia 30, na kisha madini ya jasi ambayo yanachangia asilimia 20," alifafanua Shija.
Aidha, Mhandisi Shija alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, walikuwa wamepangiwa kukusanya jumla ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 7.5, na wamefanikiwa kufikia lengo hilo la makusanyo ya mapato tangu Mei 5 mwaka huu. "Mpaka sasa tumeshakusanya Shilingi Bilioni 7.9, ambayo ni sawa na asilimia 105 ya lengo tulilopewa na Serikali," alisema Shija.
Aliongeza kuwa kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026, wameongezewa lengo na kupangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 10.5, na wanaamini kuwa kwa mwenendo mzuri wa ukuaji wa sekta ya madini ndani ya mkoa, wataweza kulifikia lengo hilo. Hii inaashiria kuwa Mkoa wa Lindi una nafasi kubwa ya kuchangia zaidi katika pato la taifa kupitia sekta ya madini katika miaka ijayo.