Taharuki imetanda katika sekta ya fedha nchini Ujerumani baada ya benki kadhaa kubwa nchini humo kuchukua hatua ya kushtukiza ya kusitisha miamala yote inayopitia mtandao maarufu wa malipo wa kimataifa, PayPal. Uamuzi huu umefikiwa kufuatia kugundulika kwa tishio kubwa la ulaghai, ambapo mamilioni ya maombi ya malipo yenye kutia shaka yalitumwa kwenye mifumo ya benki hizo.
Kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani, Süddeutsche Zeitung, benki zilianza kusitisha kuidhinisha miamala ya PayPal tangu tarehe 25 Agosti, baada ya kugundua wimbi la maombi hayo ya ulaghai wiki iliyopita. Miongoni mwa benki zilizoathirika ni pamoja na benki za majimbo ya Bavaria na Hesse, pamoja na DZ Bank, ambayo ni benki kuu ya ushirika nchini humo. Inakadiriwa kuwa thamani ya jumla ya miamala iliyozuiwa inazidi Euro bilioni 10 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania trilioni 30).
Chanzo cha tatizo hili kinaonekana kuwa ni hitilafu katika mfumo wa usalama wa PayPal wenyewe. Inaaminika kuwa mfumo huo ulishindwa kuchuja na kuzuia miamala ya kitapeli, na badala yake ukayapitisha maombi hayo ya ulaghai na kuyatuma moja kwa moja kwenda kwenye benki ili yakamilishwe. Hali hii imeibua maswali mazito kuhusu usalama wa mifumo ya malipo ya kidijitali inayotumiwa na mamilioni ya watu.
Hatua hii inatarajiwa kuleta athari kubwa nchini Ujerumani, kwani PayPal ndiyo mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao unaotumiwa zaidi nchini humo. Zaidi ya watu milioni 30 ni watumiaji wa huduma hiyo. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Rejareja ya EHI ya Ujerumani ulionyesha kuwa mwaka jana pekee, asilimia 30 ya mauzo yote yaliyofanyika mtandaoni nchini humo yalichakatwa kupitia PayPal.
Hadi sasa, haijabainika iwapo benki katika nchi nyingine za Ulaya zimechukua hatua kama hiyo. Makao makuu ya PayPal kwa bara la Ulaya yapo nchini Luxembourg, na kampuni bado haijatoa taarifa ya kina kuelezea chanzo cha hitilafu hiyo na hatua inazochukua kulinda usalama wa wateja wake. Kusitishwa kwa huduma hii kunawaacha wateja na wafanyabiashara wengi katika hali ya sintofahamu.