Katika kile kinachoonekana kama 'kukaza buti' kuelekea kilele cha mafanikio ya kiuchumi barani Afrika, Serikali ya Tanzania imetangaza azma yake nzito ya kukuza uchumi wake kufikia thamani ya Dola za Marekani Trilioni moja (takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 2,700). Mkakati huu kabambe umelenga kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa matatu bora barani Afrika yanayoongoza kwa kuvutia mitaji na uwekezaji, hatua itakayoleta mapinduzi makubwa katika ustawi wa wananchi.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, alipofanya ziara ya kikazi katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE). Ziara hiyo ililenga kukagua utendaji na kutoa dira mpya kwa taasisi hiyo kongwe, ambayo serikali inaitazama kama 'uti wa mgongo' katika kuzalisha rasilimali watu itakayosimamia mageuzi hayo ya kiuchumi.
Akizungumza kwa hisia na msisitizo, Waziri Kapinga alieleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 haitabaki kuwa maandishi tu, bali ni lazima itafsiriwe kwa vitendo kupitia taasisi imara. Alibainisha kuwa ili kufikia uchumi huo wa trilioni, Tanzania inahitaji "Kiwanda cha Maarifa" ambacho kitachakata sera, kufanya tafiti za kina, na kuzalisha wataalamu waliobobea katika masoko na teknolojia.
"Ni lazima tubadilike. Siioni CBE kama chuo cha kawaida tu, bali naiona kama 'think tank' (chemchemi ya fikra) ya wizara yetu. Tunapozungumzia Dira ya 2050, tunataka utekelezaji wake uanzie hapa. Nyinyi ndio mnaopaswa kuwa wachambuzi wakuu wa sera zetu. Tukihitaji data au mwelekeo wa soko, tunapaswa kukimbilia CBE," alisema Waziri Kapinga huku akiutaka uongozi wa chuo hicho kuongeza kasi.
Katika kusisitiza uwajibikaji, Waziri huyo aligusia miradi ya maendeleo inayoendelea chuoni hapo, akiagiza kuwa "liwe jua au mvua," miradi hiyo lazima ikamilike ndani ya muda uliopangwa kwenye mikataba. Alionya dhidi ya ucheleweshaji usio na tija, akisisitiza kuwa kila dakika inayopotea inachelewesha maendeleo ya taifa zima.
"Nimeona video nzuri ikionyesha mipango ya chuo, na nimesikiliza maelezo yenu. Matamanio yangu ni kuona haya yakitokea uhalisia haraka ili yale matunda tunayoyategemea yaanze kuonekana. Uchumi wa viwanda na ushindani unahitaji watu makini na wenye kasi," aliongeza.
Akipokea maelekezo hayo kwa niaba ya chuo, Mkuu wa CBE, Profesa Edda Lwoga, alimhakikishia Waziri kuwa chuo hicho kimejipanga kikamilifu na tayari kimeanza 'kufungua makucha' yake katika nyanja ya utafiti. Profesa Lwoga alibainisha kuwa CBE imetenga bajeti ya ndani mahususi kwa ajili ya kugharamia tafiti zinazolenga kutatua kero za kijamii na kibiashara.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, 'vichwa' vya taaluma vya CBE vimefanikiwa kukamilisha tafiti 418 na kuchapisha machapisho ya kitaluma zaidi ya 447 katika majarida yanayotambulika kimataifa na kitaifa. Hii ni ishara tosha kuwa chuo hicho hakilali usingizi katika kuhakikisha kinazalisha maarifa yanayotatua changamoto za watanzania.
"Mheshimiwa Waziri, tumejipambanua kama wadau wakubwa wa maendeleo. Ushahidi wa hili ni Mkutano wetu wa Kitaaluma wa mwaka 2025 utakaofanyika makao makuu ya nchi, Dodoma. Mkutano huu utakuwa jukwaa adhimu la kuwaleta pamoja watafiti na wabobezi kutoka ndani na nje ya nchi kujadili ustahimilivu wa uchumi," alifafanua Profesa Lwoga.
Mpango huu wa serikali kuigeuza CBE kuwa kitovu cha uchambuzi wa sera ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa Tanzania inajenga uchumi unaoongozwa na taarifa sahihi (data-driven economy), jambo ambalo ni muhimu katika ushindani wa soko la Afrika Mashariki na SADC.