Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, amewataka viongozi wa mataifa ya Afrika Mashariki kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati, ili rasilimali zilizopo zitumike kwa manufaa ya pamoja. Alitoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 11 wa Petroli wa Afrika Mashariki, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Dk. Mpango alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya nchi za Afrika Mashariki ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya sekta ya nishati, ambayo inakua kwa kasi kubwa. Aliwahimiza wawekezaji na wadau wa maendeleo kushirikiana na nchi za ukanda huo katika kuwekeza na kuboresha sekta hiyo.
"Mjadala unaofanyika katika mkutano huu unapaswa kusaidia kuboresha sera za nchi wanachama, ili sekta ya nishati iwe na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii," alisema Dk. Mpango.
Alisisitiza umuhimu wa kuhamasisha uhamaji wa haki kuelekea matumizi ya nishati safi, akionya kuwa mabadiliko haya hayapaswi kuwaacha watu nyuma, bali yanapaswa kuwanufaisha wote kwa usawa. Alibainisha kuwa rasilimali za nishati, hasa mafuta na gesi, zinaweza kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa serikali, na kusaidia uwekezaji katika miundombinu na huduma za kijamii.
Dk. Mpango alitaja rasilimali za nishati zilizogunduliwa Afrika Mashariki, ikiwemo gesi asilia nchini Tanzania, mafuta nchini Uganda, Kenya, na Sudan, methane nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na nishati ya jotoardhi nchini Tanzania na Kenya. Aliongeza kuwa maendeleo ya teknolojia ni fursa kwa nchi zinazoendelea kuongeza uwezo wa uvunaji endelevu wa nishati.
"Ni muhimu kuhakikisha kuwa mapato yanayotokana na uwekezaji huu yanatumika kwa maendeleo ya kijamii, ikiwemo kutengeneza ajira na kurejesha mazingira yaliyoharibiwa," alisisitiza.
Aidha, alihimiza kuwepo kwa sera na sheria zitakazohakikisha kuwa asilimia fulani ya mapato yatokanayo na rasilimali za mafuta yanatengwa kwa matumizi ya baadaye, ili kuhakikisha maendeleo endelevu. Alieleza kuwa hatua kubwa imepigwa katika sekta ya gesi, ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa uzalishaji katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay. Pia, ushiriki wa kampuni ya serikali ya TPDC katika kitalu cha Mnazi Bay umeongezeka kutoka asilimia 20 hadi 40, hatua inayolenga kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya nishati.