Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limezindua rasmi safari zake za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Lagos, Nigeria, hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Afrika.
Akizungumza wakati wa hafla ya kihistoria ya uzinduzi wa safari hiyo iliyofanyika tarehe 19 Septemba 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, alieleza kuwa nguvu ya kiuchumi ya Nigeria ndiyo iliyokuwa kichocheo kikuu cha uamuzi huo. Alifafanua kuwa ingawa mara nyingi Afrika Kusini hutajwa kuwa kinara wa uchumi, kuna vigezo vingine vinavyoiweka Nigeria katika nafasi ya juu, na hivyo kuifanya kuwa soko muhimu ambalo Tanzania haiwezi kulipuuza.
Profesa Kahyarara alitumia mfano wa mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa safari za Johannesburg, Afrika Kusini, akisema kuwa njia hiyo ilifungua milango mipya ya biashara kwa kiasi kikubwa. "Tumeona matokeo chanya ya kuunganisha Tanzania na Afrika Kusini. Hivi sasa, kiasi cha biashara tunachofanya na Afrika Kusini kinazidi kile tunachofanya na nchi jirani za Afrika Mashariki. Tunaamini fursa kama hizi na kubwa zaidi zipo nchini Nigeria," alisisitiza.
Mpango huu si tu kuhusu biashara ya bidhaa, bali unalenga pia sekta ya utalii na uwekezaji. Serikali inaamini kuwa kwa kurahisisha usafiri, Tanzania itavutia watalii na wawekezaji wengi zaidi kutoka Nigeria, na hivyo kupanua wigo wa masoko ya utalii nje ya yale ya jadi kutoka Ulaya na Amerika. "Huu ni mkakati wa kiuchumi wa kuimarisha utalii wa ndani ya Afrika, ambao ni endelevu zaidi," aliongeza Prof. Kahyarara.
Aidha, Katibu Mkuu huyo alithibitisha kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya anga ili kuhakikisha ATCL inaimarika. Alibainisha kuwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, fedha zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine kubwa. Vilevile, alitaja kufufua kwa ndege nne za aina ya Airbus ambazo zilikuwa zimesitisha safari kwa muda, jambo linaloongeza uwezo wa shirika hilo.
Baada ya Lagos, ATCL inajiandaa kutua katika miji mingine mikubwa Afrika Magharibi, ikiwemo Accra nchini Ghana na Abidjan nchini Ivory Coast, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa "kudaka fursa zote" katika ukanda huo na kwingineko.