Misri Yafungua Jumba la Maajabu la Trilioni 2.6: Hazina Zote za Farao Sasa Hadharani

international | Sun Nov 02 2025


Misri Yafungua Jumba la Maajabu la Trilioni 2.6: Hazina Zote za Farao Sasa Hadharani

Baada ya safari ndefu iliyochukua miongo miwili kamili, taifa la Misri hatimaye limezindua rasmi Jumba Kuu la Makumbusho la Misri (GEM - Grand Egyptian Museum), katika sherehe za kufa mtu zilizofanyika jirani kabisa na eneo maarufu la kihistoria la Piramidi za Giza na Sanamu la Sphinx.


Uzinduzi huu, uliosubiriwa kwa hamu na ulimwengu mzima, haukuwa wa kitoto. Ulitawaliwa na maonyesho ya teknolojia ya hali ya juu, ambapo mamia ya ndege zisizo na rubani (drones) zilitumika kuchora picha za miungu ya kale ya Misri na mandhari ya mapiramidi angani, huku picha za video za kuvutia za Mafarao zikionyeshwa kwenye kuta za jumba hilo jipya.


Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huu ni tumaini jipya kwa nchi hiyo. Lengo kuu ni kukuza sekta ya utalii, ambayo ni tegemeo kubwa la mapato ya fedha za kigeni (pesa taslimu) na kusaidia kuinua uchumi wa nchi ambao umekuwa ukisuasua kwa miaka kadhaa.


Uzito wa tukio hili ulithibitishwa na orodha ya wageni waliohudhuria. Rais El-Sisi aliigeuza sherehe hiyo kuwa tukio kubwa la kimataifa, akialika na kupokea wajumbe wa kifalme, marais, na mawaziri wakuu kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na Kiarabu.


Hili si jumba la makumbusho la kawaida. Limetajwa kuwa jumba kubwa zaidi duniani lililojengwa mahususi kwa ajili ya kuhifadhi na kuonyesha historia ya ustaarabu mmoja tu. Lina jumla ya vizalia (artifacts) zaidi ya 50,000. Kwa kulinganisha, Jumba maarufu la Louvre huko Paris, Ufaransa, lina maonyesho takribani 35,000 ya tamaduni mbalimbali.


Katika hotuba yake, Rais El-Sisi alisema, "Tunataka jumba hili liwe jukwaa la kimataifa la mazungumzo, kubadilishana maarifa, na kongamano la tamaduni za binadamu. Litakuwa nembo na mwanga kwa wote wanaopenda maisha na kuamini katika thamani ya utamaduni wa mwanadamu."


Mradi huu wa GEM ni moja ya miradi mikuu ya kitaifa ya Rais El-Sisi tangu aingie madarakani mwaka 2014, ikiwa ni mkakati wa kufufua uchumi ulioathiriwa tangu mapinduzi ya "Arab Spring" ya mwaka 2011.


Kivutio kikubwa zaidi kwa watalii kinatarajiwa kuwa mkusanyiko kamili wa hazina zilizopatikana kwenye kaburi la Farao kijana, Tutankhamun. Tangu kaburi hilo maarufu ligunduliwe mwaka 1922, hii ni mara ya kwanza kwa vitu vyake vyote, vikiwemo kinyago chake maarufu cha dhahabu, kuonyeshwa pamoja katika sehemu moja.


Jumba hili jipya linachukua nafasi ya lile la zamani lililopo katikati ya jiji la Cairo, ambalo lilijengwa zaidi ya miaka 100 iliyopita. Jumba la zamani lilikuwa limeelemewa na maelfu ya vizalia, kiasi cha kufananishwa na "ghala" kutokana na msongamano na ukosefu wa maelezo ya kutosha kwa vitu vingi. Jumba jipya la GEM ni la kisasa, lina nafasi kubwa na linatumia teknolojia kama vile maonyesho ya uhalisia pepe (virtual reality) ili kutoa uzoefu bora kwa wageni.


Safari ya ujenzi haikuwa rahisi. Mradi ulianza rasmi mwaka 2005 chini ya utawala wa Rais Hosni Mubarak, kwa gharama iliyokadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 1 (takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.6). Hata hivyo, ujenzi ulisimama kufuatia ghasia za umma zilizomwondoa Mubarak madarakani mwaka 2011. Baada ya kuchelewa mara kwa mara, hata tarehe ya uzinduzi iliyopangwa majira ya joto mwaka huu ililazimika kusogezwa mbele tena kufuatia mivutano ya kivita iliyotokea katika ukanda wa Mashariki ya Kati mwezi Juni.


Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Misri, Sharif Fathi, alisema serikali inatarajia jumba hili kuvutia zaidi ya wageni milioni 5 kwa mwaka. Hii italiweka katika viwango sawa na majumba maarufu zaidi duniani. Kwa mfano, mwaka 2024, Louvre ilipokea wageni milioni 8.7, Jumba la Makumbusho la Uingereza (British Museum) lilipata wageni milioni 6.5, na Jumba la Metropolitan la New York lilipata wageni milioni 5.7.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.