Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa, amewataka vijana mkoani humo na nchi nzima kuamka kutoka katika usingizi wa kusubiri ajira za ofisini na badala yake wageukie sekta ya ujuzi na kazi za mikono, akisisitiza kuwa huko ndiko kuliko na "fedha ndefu" inayozidi hata mishahara ya waajiriwa wengi serikalini na sekta binafsi.
Akizungumza kwa lugha ya picha na uhalisia wakati akifungua Kongamano Maalum la Utekelezaji mkoani Kagera leo, ambalo limewakutanisha wazawa na wadau wa maendeleo kujadili mustakabali wa uchumi wa mkoa huo, RC Mwassa amesema wakati umefika wa kubadili mtazamo wa nini maana ya "kazi."
Kiongozi huyo, ambaye hafichi ukweli, alitumia mfano hai wa sekta ya urembo na mitindo, akibainisha jinsi utandawazi ulivyotengeneza fursa za ajabu kwa vijana waliochangamka. Alieleza kuwa maisha ya sasa yamebadilika kiasi kwamba hata huduma ndogo ambazo zamani zilifanyika nyumbani bure, sasa ni biashara inayolipa.
"Ndugu zangu, utandawazi umetulemaza kidogo, lakini huo ulemavu wa baadhi ndio fursa kwa wengine. Leo hii, mwanamke hawezi hata kujipaka wanja mwenyewe, anatafuta mtu amfanyie 'makeup'. Hii ni biashara," alisema RC Mwassa huku akisisitiza hoja yake kwa mahesabu ya haraka.
Alifafanua kuwa kijana mwenye ujuzi wa kupamba (makeup artist) anaweza kutoza kuanzia Shilingi 10,000 kwa kichwa kimoja. "Ukipata wateja watano tu kwa siku, tayari una Shilingi 50,000 mfukoni. Hiyo ni pesa ambayo mtu wa ofisini anaweza asipate kwa siku. Sasa, ukiongeza na ujuzi wa kusuka nywele, hesabu inabadilika kabisa. Kijana anaweza kuingiza hadi Shilingi Laki Tatu (300,000) kwa siku moja. Huyu unamlinganishaje na mtu anayesubiri mwisho wa mwezi?" alihoji Mwassa.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa inakuja wakati ambapo takwimu zinaonesha kuwa sekta isiyo rasmi ndiyo mwajiri mkubwa zaidi nchini Tanzania. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya vijana wengi kudharau kazi za mikono kama ufundi, ususi, na kilimo, wakiamini kuwa mafanikio yanapatikana kwenye viyoyozi pekee.
Katika kuhakikisha vijana wa Kagera hawaachwi nyuma katika mageuzi haya ya kiuchumi, RC Mwassa ametangaza kuandaliwa kwa Kongamano Kubwa la Vijana hivi karibuni. Jukwaa hilo litalenga kuwajengea uwezo wa kujitambua (Self-realization) na kuwahamasisha kuunda vikundi vya kiuchumi ili warasimishe shughuli zao.
"Tunataka vijana wa Kagera wamiliki uchumi wao. Sio tu wawe watazamaji au vibarua, bali wamiliki wa biashara na kampuni zinazotokana na ujuzi walionao. Fursa zipo, kinachokosekana ni uthubutu na mwelekeo sahihi, na hilo ndilo tunaloenda kulifanyia kazi," alihitimisha.
Mkoa wa Kagera, uliopo mpakani mwa nchi za Uganda, Rwanda na Burundi, una fursa nyingi za kibiashara ambazo zikitumiwa vyema na vijana wenye ujuzi, zinaweza kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha uchumi katika ukanda wa Ziwa Victoria.