Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, ameipa Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) jukumu la kushughulikia kwa dharura changamoto zinazoletwa na ukuaji wa haraka wa miji nchini. Waziri ameagiza baraza hilo kuhakikisha kunakuwepo na mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kukabiliana na athari za ukuaji huo.
Mhandisi Masauni aliyasema hayo jana jijini Dodoma wakati akizindua bodi ya tisa ya NEMC, ambayo itaongozwa na Mkuu wa Mkoa mstaafu, Mhandisi Mwanasha Tumbo. Alieleza kuwa miji mingi nchini inakua kwa kasi kubwa bila kuwa na mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi, hali ambayo inasababisha msongamano wa watu, uchafuzi wa mazingira, ukosefu wa mifumo bora ya maji safi na usimamizi wa taka, pamoja na uharibifu wa vyanzo vya maji na kingo za mito na bahari.
Aidha, Waziri Masauni aliagiza bodi hiyo kuhakikisha inafanya vikao vyake kwa mujibu wa sheria na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha inajitegemea kifedha. “Nawaagiza mshirikiane kwa karibu na menejimenti ya Baraza ili kuleta matokeo yenye tija na msimamie vizuri Baraza ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira nchini,” alisisitiza Waziri.
Pia, aliwataka wajumbe wa bodi kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira, akieleza kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa uelewa miongoni mwa wananchi kuhusu masuala haya. Alisema ukosefu wa elimu ya mazingira kwa wananchi unachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli zinazoharibu mazingira, kama vile ukataji miti holela, uchomaji misitu, na utupaji taka ovyo.
“Hakikisheni Baraza linakuwa mamlaka ya kweli ya usimamizi wa mazingira nchini na linakabiliana ipasavyo na mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa joto duniani, kupungua kwa mvua au mvua zisizotabirika, na majanga kama mafuriko au ukame, ambayo yote yanachangia kuharibu mazingira na rasilimali zetu za asili,” aliongeza Waziri Masauni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi, alieleza kuwa baraza hilo limekuwa likifanya uchunguzi muhimu unaosaidia katika usimamizi na uhifadhi bora wa mazingira. Pia, wamekuwa wakiratibu tafiti mbalimbali kuhusu mazingira ili kukusanya na kusambaza taarifa muhimu kuhusu matokeo ya tafiti hizo.
Dk Semesi alisema NEMC imekuwa ikipitia kwa umakini taarifa za tathmini ya athari za mazingira (EIA) na kutoa mapendekezo kuhusu utoaji wa vibali kwa kampuni zinazotekeleza miradi mbalimbali nchini. Aliongeza kuwa NEMC imekuwa ikibainisha aina za miradi na programu zinazohitaji kufanyiwa uhakiki wa mazingira chini ya Sheria ya EIA na kusimamia udhibiti na utekelezaji wa viwango vya ubora wa mazingira kitaifa.
“NEMC imekuwa ikianzisha na kubuni taratibu na kinga za kuzuia ajali zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira, na pia kubuni hatua za marekebisho pindi ajali zinapotokea. Vilevile, tumeanzisha programu zinazolenga kuendeleza elimu ya mazingira na elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa usimamizi mwafaka wa mazingira,” alisema Dk Semesi.
Alifafanua kuwa NEMC imekuwa ikichapisha na kusambaza vitabu vya miongozo, kanuni za kisheria, na miongozo mingine kuhusu usimamizi wa mazingira na njia za kuzuia au kupunguza uharibifu wa mazingira. Alimalizia kwa kusema kuwa NEMC inatoa ushauri wa kitaalamu kwa vyombo mbalimbali vinavyohusika na usimamizi wa maliasili na mazingira ili kuviwezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, pamoja na kutekeleza kazi nyinginezo zinazotolewa na Waziri mwenye dhamana ya mazingira.