Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, ametoa wito kwa Watanzania wote kuacha kutumia nishati chafu na badala yake kutumia nishati safi ya kupikia. Alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda mazingira, na kuhifadhi viumbe hai.
Masauni aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati wa futari aliyoiandaa kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa ajili ya kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa mazingira. Alisisitiza kuwa juhudi za kulinda mazingira hazifanywi kwa ajili ya manufaa ya sasa tu, bali pia kwa ajili ya vizazi vijavyo.
"Tunapozungumzia mazingira, hatufanyi haya kwa ajili yetu tu, bali kwa watoto na wajukuu zetu. Ni muhimu kushirikiana, kufanya kazi pamoja, na kufanya maamuzi yanayonufaisha mazingira na watu wanaoyategemea," alisema Masauni.
Aliongeza kuwa wadau mbalimbali wana jukumu la kuunda dunia endelevu na yenye uwiano kwa wote. Alisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali zilizopo ili ziweze kuendelea kuwepo kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kila mtu anapaswa kuzingatia athari za matendo yake, hata madogo kiasi gani, kwenye mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, alieleza kuwa kazi inayofanywa na wadau katika kuhifadhi mazingira ni muhimu kwa kutimiza maandiko ya vitabu vitakatifu. Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na maliasili na mifumo ikolojia ya kipekee, hivyo ni muhimu kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti shughuli za binadamu zinazoharibu mazingira.
"Tunapaswa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti shughuli za binadamu kama uchimbaji madini, ufugaji na kilimo visivyo endelevu, na ukataji mkubwa wa misitu," alisema Dk. Semesi.
Aliongeza kuwa juhudi za pamoja zinahitajika ili kupunguza au kumaliza uharibifu huo. Serikali kupitia NEMC inafanya kazi kufikia lengo hilo. Alizungumzia pia Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka, ambayo itaadhimishwa Machi 28-30, 2025, jijini Dar es Salaam.
Dk. Semesi alisema kuwa maadhimisho hayo yataleta pamoja wadau wa mazingira ili kuangazia umuhimu wa usimamizi endelevu wa taka na kukuza uchumi mzunguko. Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Kufikia lengo la taka sifuri katika masuala ya mitindo na nguo" na kauli mbiu ya Kitaifa ni "TAKA NI FURSA". Alisisitiza kuwa maadhimisho hayo yatakuwa fursa ya kuimarisha ushirikiano katika kutafuta suluhisho la changamoto za kimazingira.
Aliongeza kuwa serikali imepiga hatua katika kulinda mazingira kwa kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii, kuweka mikakati ya kuhakikisha sheria za mazingira zinafuatwa, kufanya tafiti za mazingira, kusaidia uhamasishaji na elimu kwa umma, na kutambua kuwa mazingira ni suala mtambuka linalohitaji ushiriki wa sekta zote.