Wananchi wanatarajia kuona mabadiliko yanayoonekana katika maisha yao, hasa katika sekta muhimu ya afya, kama ishara ya mafanikio ya juhudi zinazofanywa kuelekea maendeleo endelevu. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, alisisitiza umuhimu wa mabadiliko hayo wakati akielezea kuhusu maadhimisho ya wiki ya afya nchini. Maadhimisho haya yanaendelea kufanyika kwa matukio mbalimbali yanayoangazia sekta ya afya kote nchini.
Dkt. Mollel alieleza kuwa uboreshaji unaoendelea katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma bora, upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya matibabu, na uwekezaji katika miundombinu, ndio mabadiliko chanya ambayo wananchi wanayatarajia. Aliongeza kuwa maendeleo haya ni ushahidi wa wazi wa juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.
Alifurahia kutangaza kuwa mwaka huu maadhimisho ya wiki ya afya yanafananyika wakati nchi imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vinavyohusiana na uzazi, vifo vya mama na mtoto, pamoja na kupungua kwa idadi ya wagonjwa wanaohitaji kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Mafanikio haya yanaonyesha juhudi za pamoja za serikali na wadau mbalimbali katika sekta ya afya.
Zaidi ya hayo, Dkt. Mollel alifichua mafanikio mengine makubwa, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa vifo vinavyosababishwa na saratani kwa asilimia 78. Alisema mafanikio haya yamewezekana kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanywa, hasa katika mfumo wa uchunguzi wa haraka wa magonjwa hayo. Alieleza kuwa tofauti na zamani, ambapo vipimo vya saratani vilichukua muda mrefu kutoa majibu, sasa teknolojia imewezesha kugundua saratani mapema, hivyo kuruhusu wagonjwa kuanza matibabu kwa wakati. Hii ni hatua kubwa imepigwa katika kuboresha afya za wananchi na kupunguza mzigo wa magonjwa nchini.