Katika onyesho la kipekee la upendo na mshikamano, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Rwepa’s iliyopo Manispaa ya Kahama, wamejenga daraja la matumaini kwa kuwatembelea na kuwafariji wenzao wanaoishi katika mazingira magumu kwenye kituo cha New Hope. Ujumbe wao mkuu ulikuwa mmoja: mazingira mnayotoka yasifafanue hatima yenu; elimu ndiyo ufunguo wa kutimiza ndoto zenu.
Akiongoza ujumbe huo, Dorce Fulgency, mwanafunzi wa kidato cha nne, alizungumza kwa hisia akisema kuwa hali ya kuwa yatima au kutelekezwa haipaswi kuwa pingu ya kuwazuia kufikia kilele cha mafanikio. Aliahidi kuwa, pindi atakapohitimu masomo yake na kupata fursa, atarejesha shukrani kwa jamii kwa kuwashika mkono watoto wengine wenye uhitaji. "Changamoto hizi zisiwe mwisho, bali ziwe mwanzo wa kuandika historia yenu ya ushindi," alisema Dorce.
Wazo hilo liliungwa mkono na Rehema Malima wa kidato cha tatu, ambaye aliongeza kuwa ndoto za kuwa madaktari, wahandisi, au viongozi mashuhuri haziwezi kuzimwa na ugumu wa maisha ya sasa. Alisisitiza kuwa kinachohitajika ni nia ya dhati na bidii isiyokoma katika masomo.
Kwa upande wao, wenyeji wa kituo cha New Hope walionyesha ukomavu na ujasiri mkubwa. Joseph Sospeter, mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni hapo, alitoa kauli iliyogusa wengi: "Wengi hudhani yatima hawawezi kufaulu, sisi tunasema tunaweza na tutafaulu. Tumejifunza kutoyaogopa maisha, bali tuyakabili kwa maarifa na nidhamu." Aliomba wadau wengine wajitokeze kuwasaidia, hasa kwa mahitaji ya vifaa vya shule ambavyo ni muhimu katika safari yao ya elimu.
Uongozi wa shule ya Rwepa’s, kupitia Mkurugenzi wake Frank Samweli, uliunga mkono kwa vitendo juhudi za wanafunzi wake. Walikabidhi msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo kilo 70 za mchele, lita 20 za mafuta ya kupikia, sabuni, kalamu, na soda, kama ishara ya upendo na kuwatia moyo.
Mmiliki wa kituo hicho, Suleiman Juma, aliwashukuru wanafunzi hao kwa kitendo chao cha kiungwana, akisema kimewapa watoto wake imani mpya na kuwathibitishia kuwa hawako peke yao. Alieleza kuwa watoto hao wamekuwa wakipata maendeleo makubwa kitaaluma, wakiamini elimu ndiyo urithi pekee wenye thamani ya kudumu.