Kwa miaka mingi, wanafunzi katika baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Mji wa Handeni, mkoani Tanga, wamelazimika kuanza safari ya miguu alfajiri na mapema, wakitembea umbali wa kilometa 22 kila siku kwenda na kurudi Shule ya Sekondari Kwenjugo kusaka elimu. Hata hivyo, adha hiyo sasa imefikia tamati baada ya serikali kukamilisha ujenzi wa Shule ya kisasa ya Amali ya Mapinduzi.
Mradi huu wa kihistoria, ulioigharimu serikali zaidi ya Shilingi milioni 584.2 kupitia Mpango wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), unatajwa kuwa mapinduzi halisi katika sekta ya elimu ndani ya halmashauri hiyo. Kukamilika kwa shule hii sio tu kwamba kunapunguza utoro na uchovu kwa wanafunzi, bali pia kunatarajiwa kuongeza ari ya kujifunza na kuinua kiwango cha ufaulu.
Akikagua mradi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, alitoa shukrani za dhati kwa serikali kwa kuwezesha ujenzi huo, akisema ni uthibitisho wa dhamira yake ya kusogeza huduma bora za elimu karibu na wananchi. "Nawapongeza wasimamizi wote, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwenjugo, John Rajabu, na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Hadija Kingimali, kwa kazi nzuri. Tumewaondolea watoto wetu mzigo mzito na sasa wanaweza kuelekeza nguvu zao zote masomoni," alisema Ukwaju.
Ili kuifanya shule hiyo kuwa kituo kamili cha malezi, Mkurugenzi Ukwaju ameagiza kufanyika kwa tathmini ya haraka ili eneo la shule lipanuliwe na kupata viwanja vya michezo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Hadija Kingimali, shule hiyo mpya ina miundombinu ya kisasa inayoweza kuhudumia wanafunzi 320 kwa wakati mmoja. Alithibitisha kuwa shule zitakapofunguliwa rasmi Septemba 15, kundi la kwanza la wanafunzi 53 wa kidato cha kwanza litaingia rasmi na kuanza masomo katika mazingira mapya na bora zaidi.
Ujenzi wa shule hii, ulioanza Septemba 27, 2024, umehusisha majengo 13, yakiwemo maabara za kisasa za Kemia na Biolojia pamoja na jengo maalum la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hatua itakayowapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo.