Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimefanya tukio la kihistoria kwa kumtunuku Shahada ya Heshima ya Falsafa ya Sayansi, Dkt. Akinwumi Adesina, Rais anayemaliza muda wake wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Tuzo hii ilitolewa na Mkuu wa Chuo hicho, ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wakati wa Mahafali ya 55, duru ya kwanza, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Tukio hili lilisisitiza umuhimu wa mchango wa Dkt. Adesina katika maendeleo ya Afrika na dunia nzima, hususan katika sekta za kilimo na fedha. Profesa Rwekaza Mukandala, akisoma wasifu wa Dkt. Adesina kabla ya kutunukiwa shahada hiyo, alieleza kuwa Dkt. Adesina ni kielelezo halisi cha mchanganyiko adimu wa elimu bora, uongozi wenye maono, na athari chanya zenye kugusa maisha ya watu. Hizi ndizo sifa kuu zilizomfanya astahili kutambuliwa kwa heshima hii kubwa.
UDSM ina utaratibu wa kutoa shahada za heshima kila baada ya miaka mitatu kwa watu mashuhuri wenye sifa za kipekee na waliotoa mchango mkubwa kwa jamii. Dkt. Adesina, ambaye ana Shahada ya Uzamivu ya Uchumi wa Kilimo, amepongezwa kwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, uchumi, na fedha barani Afrika. Profesa Mukandala alitoa mfano wa uongozi wake alipokuwa Waziri wa Kilimo nchini Nigeria kuanzia mwaka 2011. Wakati huo, Dkt. Adesina alianzisha mikakati bunifu, ikiwemo mpango wa "e-wallet" (mkoba wa kielektroniki), ambao uliwezesha wakulima kupokea ruzuku ya mbolea kupitia simu zao za mkononi. Mpango huu ulipunguza kwa kiasi kikubwa urasimu na rushwa, ukinufaisha zaidi ya wakulima milioni 11 na kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini Nigeria.
Baada ya kuchukua nafasi ya Urais wa AfDB mwaka 2015, Dkt. Adesina aliongoza benki hiyo kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi. Chini ya uongozi wake, mtaji wa benki ulipanda kwa kasi kutoka Dola za Kimarekani bilioni 93 (takriban Shilingi trilioni 232.5 za Tanzania) mwaka 2015, hadi Dola za Kimarekani bilioni 208 (takriban Shilingi trilioni 520 za Tanzania) kufikia mwaka 2019. Alianzisha vipaumbele vitano vikuu vinavyojulikana kama "High 5s": Kuangaza na kuipa nishati Afrika, kulisha Afrika, kuongeza viwanda Afrika, kuiunganisha Afrika, na kuboresha maisha ya Waafrika. Vipaumbele hivi vimetajwa kuwa na athari chanya kwa zaidi ya watu milioni 565 barani Afrika.
Profesa Mukandala alifafanua zaidi kuwa wakati wa uongozi wa Dkt. Adesina, AfDB imekuwa benki inayoongoza katika ufadhili wa miradi ya miundombinu, ambapo zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 55 (takriban Shilingi trilioni 137.5 za Tanzania) zimetumika kuwekeza katika sekta hiyo barani kote. Aidha, benki hiyo iliwekeza pakubwa katika miradi ya usalama wa chakula, na inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 100 walinufaika. Kwa upande wa afya, AfDB ilitoa Dola za Kimarekani bilioni 3 (takriban Shilingi trilioni 7.5 za Tanzania) kuboresha sekta hiyo barani Afrika, na kiasi kama hicho kilitumika kuimarisha sekta ya dawa.
Katika mageuzi ya kifedha, Dkt. Adesina amechangia pakubwa kubadilisha mifumo ya kifedha barani Afrika ili iwe jumuishi na kuwanufaisha makundi yote, ikiwemo vijana, wanawake, na wakazi wa vijijini. Akiwa Rais wa AfDB, alisanifu upya mifumo ya ufadhili wa maendeleo, ikiwemo kuongeza mtaji wa benki, kuzindua hati fungani za kijamii, na kuanzisha mifuko ya dharura ya kukabiliana na majanga. Hatua hizi zimeimarisha miradi muhimu katika sekta za miundombinu, afya, kilimo, na nishati barani Afrika.
Mchango wa AfDB Tanzania Chini ya Uongozi wa Dkt. Adesina
Kwa upande wa Tanzania, chini ya uongozi wa Dkt. Adesina, AfDB imekuwa na ushirikiano mzuri na Serikali ya Tanzania, ikilenga kuimarisha miundombinu, kujenga uchumi shindani, na kuboresha sekta binafsi kwa ajili ya kuzalisha ajira. Katika sekta ya miundombinu, AfDB imesaidia miradi mikubwa ya usafiri wa ardhini, majini, na angani. Mifano mashuhuri ni pamoja na mradi wa Barabara ya Mzunguko jijini Dodoma, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), hususan kipande kinachounganisha Tanzania na Burundi.
Katika kukuza sekta binafsi, AfDB imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika kuimarisha sekta ya kilimo, ambayo imeiwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128. Vilevile, AfDB inashirikiana na Tanzania katika kuendeleza Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), ambao umewawezesha vijana zaidi ya 11,000 kujishughulisha na kilimo cha kisasa nchini.
Baada ya kupokea Shahada hiyo ya Heshima, Dkt. Adesina alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaliko wa kuja Tanzania, nchi anayoipenda na anayoitaja kuwa "nyumbani kwake." Pia, alikishukuru Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa heshima kubwa waliyompatia na kuwatia moyo wahitimu wengine takriban 842 waliotunukiwa shahada pamoja naye, kuutumia maarifa waliyoyapata kubuni mikakati itakayopeleka Bara la Afrika mbele.