Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limepokelewa kwa shangwe kubwa liliporejea nchini baada ya kutwaa Tuzo ya European Award for Quality Choice Achievement 2025. Tuzo hiyo ya kifahari ilitolewa katika sherehe zilizofanyika jijini Stockholm, Sweden, ikiashiria kutambuliwa kwa ubora wa huduma zinazotolewa na shirika hilo.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ulishuhudia nderemo na vifijo vya aina yake wakati timu ya TANAPA ilipowasili ikiwa imeshika tuzo hiyo. Mapokezi yao yaliambatana na kaulimbiu iliyosomeka, “TANAPA Nyumbani kwa Tuzo,” ikionyesha furaha na fahari ya taifa kwa mafanikio hayo.
Tuzo hii ya heshima imetolewa na taasisi mashuhuri ya European Society for Quality (ESQR), ambayo inafanya tathmini ya viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali duniani. Ushindi huu unaonesha kuwa TANAPA inazingatia viwango vya juu vya kimataifa katika utendaji wake.
Timu ya TANAPA, iliyoongozwa na Kamishna wa Uhifadhi CPA (T) Musa Nassoro Kuji, ilipokelewa kwa heshima kubwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau muhimu katika sekta ya utalii, watumishi wa TANAPA, na wananchi kwa ujumla. Mapokezi haya yalikuwa ishara ya wazi ya fahari ya kitaifa kwa mafanikio haya ya TANAPA.
Akizungumza mara baada ya kuwasili nchini, Kamishna Kuji alisema: “Tuzo hii si yetu pekee, bali ni ya Watanzania wote. Kupokea tuzo hii kwa mara ya sita mfululizo ni uthibitisho tosha wa dhamira yetu ya kuendelea kutoa huduma bora katika hifadhi zetu zote 21 za Taifa. Watalii hawaji Tanzania kwa bahati nasibu; wanakuja kwa sababu ya ubora wa hifadhi zetu na huduma tunazowapa. Tunaahidi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa vivutio vyetu ili Tanzania iendelee kupendwa, kutembelewa, na kuheshimiwa duniani kote.”
Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Bi. Steria Ndaga, ambaye pia ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, alisisitiza kuwa mafanikio haya yametokana na ushirikiano mzuri na mshikamano wa wadau wote wanaohusika na sekta ya utalii, ikiwa ni pamoja na serikali, TANAPA yenyewe, na wananchi wote kwa ujumla. Alisema kuwa umoja huu ndio umewezesha TANAPA kufikia mafanikio haya makubwa.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Bwana Godwell Meng’ataki, ambaye pia ni Mkuu wa Kanda ya Kusini na alikuwa miongoni mwa timu iliyosafiri kwenda Stockholm, amesema kuwa ushindi huu ni ishara ya ushindani mkubwa uliopo katika ngazi ya kimataifa. Alifurahia kuwa TANAPA iliweza kuibuka mshindi kati ya taasisi nyingi kutoka zaidi ya nchi 42 zilizoshiriki.
“Ushindi huu sio tu heshima kubwa kwa shirika letu, bali pia ni mwaliko mpya kwa dunia nzima kuendelea kuitembelea Tanzania na kujionea uzuri wa hifadhi zetu na ukarimu wa watu wetu. Tumepata fursa ya kujifunza mengi kutoka kwa taasisi nyingine duniani, na sasa tuko tayari kwenda mbali zaidi katika kuboresha huduma zetu,” alisisitiza Bwana Meng’ataki.
Kwa miaka sita mfululizo, kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, TANAPA imekuwa ikipokea tuzo hii ya ubora wa huduma katika ngazi ya kimataifa. Mafanikio haya yameipa Tanzania sifa ya kipekee katika sekta ya utalii barani Afrika na duniani kote, na kuifanya kuwa moja ya maeneo yanayopendekezwa zaidi kwa watalii wanaotafuta uzoefu wa kipekee wa asili na wanyamapori.