Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Doroth Gwajima, amesema serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha inatokomeza changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
Hayo yameelezwa leo wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Mdahalo huo ulifanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani, ambayo yatafanyika kitaifa Aprili 12, 2025, mkoani Mtwara.
Dkt. Gwajima amewataka wazazi wanaofikia hatua ya kutengana, kuwatumia maofisa ustawi wa jamii ili kukaa meza moja na kupata muafaka kuhusu malezi ya watoto. Pia, amewahimiza wananchi kutumia vizuri maofisa maendeleo ya jamii ili kupata suluhisho la migogoro mbalimbali inayojitokeza kwenye familia.
Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa maofisa hao ili waweze kutumia utaalamu wao kukabiliana na migogoro mbalimbali, hasa talaka, ambayo imetajwa kuwa chanzo kikubwa cha watoto kuishi mtaani na kufanyishwa kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amesema mkoa huo una jumla ya watoto takribani 90 wanaoishi na kufanya kazi mtaani, ambapo asilimia kubwa ni watoto wa kiume. Takwimu hizo ni za watoto ambao tayari wameshafikiwa, lakini anaamini kuwa kuna watoto wengine ambao hawajafikiwa na hawapo kwenye takwimu hizo.
"Miongoni mwa changamoto zinazopelekea uwepo wa watoto hao katika mkoa wetu ni pamoja na talaka holela, ambazo zimekuwa sababu kubwa ya watoto kukosa malezi bora, na baadhi ya watoto kupelekwa kwa bibi ambao nao wanahitaji kuhudumiwa, na baadhi ya familia kutokuipa elimu kipaumbele," amesema Kanali Sawala.
Hata hivyo, ili kukabiliana na changamoto hiyo na kutambua umuhimu wa mtoto kwa mkoa na taifa kwa ujumla, mkoa umechukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha watoto na huduma za marekebisho ya tabia, kuwapeleka kwenye vituo vya kulelea watoto, na kuwaunganisha na familia zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Saidi Nyengedi, amesema uwepo wa watoto hao ni kosa la wazazi kwa kutozingatia umuhimu wa malezi. Amesema wazazi wakizingatia umuhimu wa malezi, hakuna mtoto atakayeishi na kufanya kazi mtaani.
"Mimi nakataa wazazi wanaonyooshea vidole kwa kusema watoto wa sikuhizi. Mimi nasema wazazi na walezi wa sikuhizi ndio wenye matatizo, maana wao wakichukua jukumu lao, hapatakuwa na mtoto wa mtaani. Mtoto aliyetelekezwa wala siyo unyanyasaji wa kijinsia, ila tatizo tunalo sisi wazazi," amesema Nyengedi.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni 'Imarisha Ushirikiano Kuzuia Watoto Kuishi Mtaani'.