'Nimeanza Maisha Mapya' - Ushuhuda Waleta Tumaini Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya

culture | Thu Jun 26 2025


'Nimeanza Maisha Mapya' - Ushuhuda Waleta Tumaini Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya

"Nilikuwa nimepoteza kabisa mwelekeo wa maisha yangu. Matumizi ya dawa yalikuwa yamenifanya nihisi kama maisha yangu hayana tena maana. Lakini sasa ninafanya kazi, nimekuwa baba bora kwa watoto wangu, na nimeanza maisha mapya." Maneno haya ya Amki (si jina lake halisi) yaligusa mioyo ya wengi na kuleta tumaini jipya wakati wa kilele cha maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya, yaliyofanyika jijini Dodoma.


Ushuhuda wa Amki ni matokeo halisi ya jitihada zinazofanywa na washirika mbalimbali, ikiwemo shirika la Amref Health Africa – Tanzania, ambalo kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia mpango wa PEPFAR na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC Tanzania), linatekeleza miradi ya kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya.


Katika maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu "Wekeza kwenye Kinga na Tiba Dhidi ya Dawa za Kulevya," Amref ilipata fursa ya kuonyesha kazi kubwa inayofanya visiwani Zanzibar. Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Zanzibar na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA), Amref inatoa huduma ya Tiba Mbadala (MAT) katika kituo cha Kidongo Chekundu. Huduma hii imekuwa mkombozi, ikiwapa waraibu tiba salama, ushauri nasaha, na fursa ya kujikinga na maambukizi ya VVU yanayoweza kusababishwa na matumizi ya sindano zisizo salama.


Kwenye banda lao la maonyesho katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, wananchi na viongozi walipata elimu kuhusu safari ya uponyaji ya waraibu. Mkurugenzi wa Miradi kutoka U.S CDC Tanzania, Dk. George Mgomela, alitembelea banda hilo na kuelezwa kwa kina kuhusu mafanikio ya programu hiyo, ambayo ni sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI visiwani.


Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika kinga na tiba. Alitoa wito kwa wadau wote kuunganisha nguvu ili kutokomeza janga hili nchini. "Ni muhimu kuendeleza juhudi za pamoja, za kina na endelevu ili kuhakikisha mafanikio ya kudumu katika afya na ustawi wa jamii," alisema Waziri Mkuu.


Kama ishara ya kutambua mchango wao, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, aliikabidhi Amref Tanzania cheti maalum cha ushiriki. Ushuhuda kama wa Amki unathibitisha kuwa kwa uwekezaji sahihi katika tiba na msaada wa kisaikolojia, vita dhidi ya dawa za kulevya inaweza kushinda na maisha yaliyopotea yanaweza kurejeshwa.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.