NEEMA YA HUDUMA ZA BINGWA SERENGETI: DC Marko Atoa Ahadi Nzito, Asema 'Hakuna Mgonjwa Atakayekosa Nauli ya Kwenda Ocean Road'

culture | Thu Dec 11 2025


NEEMA YA HUDUMA ZA BINGWA SERENGETI: DC Marko Atoa Ahadi Nzito, Asema 'Hakuna Mgonjwa Atakayekosa Nauli ya Kwenda Ocean Road'

Wakazi wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamepata faraja ya kipekee baada ya Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), kusogeza huduma za kibingwa za uchunguzi wa saratani mlangoni mwao. Hatua hii imetajwa kuwa ni mapinduzi makubwa katika sekta ya afya, ikilenga kuwafikia wananchi wa pembezoni ambao kwa muda mrefu walilazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 1,000 kufuata huduma hizo jijini Dar es Salaam.


Akihitimisha kambi maalum ya siku tatu ya "Huduma za Mkoba" iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Angelina Marko, amemwaga sifa lukuki kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuhakikisha huduma za afya hazibaki mijini pekee. DC Marko amesema kampeni hiyo ni kielelezo tosha cha jinsi serikali inavyojali uhai wa kila Mtanzania, bila kujali kipato wala mahali anapoishi.


Katika kile kilichoibua shangwe na matumaini mapya kwa wananchi, DC Angelina Marko ametoa tamko zito la kiofisi akiahidi kuwa Serikali ya Wilaya itabeba jukumu la kuwasafirisha wagonjwa wote watakaopewa rufaa kwenda Taasisi ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.


“Nataka niwahakikishie wananchi wangu, hakuna mgonjwa wa Serengeti atakayekufa au kuteseka kwa kukosa nauli ya kwenda Ocean Road. Hilo lisiwatie hofu. Serikali yenu ipo macho na itagharamia usafiri ili kila aliyepewa rufaa akapate matibabu stahiki na kuokoa maisha yake. Hii ndiyo maana halisi ya Rais Samia kusema ‘Kazi Iendelee’ kwa vitendo,” alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya kwa sauti ya kiamri na huruma.


Kwa upande wa takwimu za kitaalamu, Daktari Bingwa wa Saratani na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka ORCI, Dkt. Crispin Kahesa, ametoa tathmini ya kina kuhusu mwitikio wa kampeni hiyo iliyofanyika katika wilaya mbili za kanda ya ziwa; Bukombe na Serengeti. Dkt. Kahesa amebainisha kuwa jumla ya wananchi 927 wamejitokeza kupima afya zao, jambo linaloashiria kuongezeka kwa mwamko wa jamii kuhusu umuhimu wa kugundua magonjwa mapema.


Akichambua takwimu hizo, Dkt. Kahesa alisema: “Katika Wilaya ya Bukombe, tuliwapima wananchi 379, ambapo tisa walibainika kuwa na viashiria vya awali na kuanzishiwa matibabu hapo hapo, huku watatu wakipewa rufaa. Hapa Serengeti, mwitikio ulikuwa mkubwa zaidi ambapo tumewapima watu 548. Kati yao, 18 walionekana na dalili za awali na kupatiwa tiba, na wagonjwa wawili wamepewa rufaa ya kwenda Ocean Road kwa uchunguzi na tiba zaidi.”


Dkt. Kahesa alisisitiza kuwa dhana ya kwamba matibabu ya saratani ni ya matajiri tu haina nafasi, kwani ORCI inatoa huduma kulingana na uwezo wa mgonjwa na serikali imeweka mifumo ya kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.


Naye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Johanece Bakuba, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya, amesema mafanikio ya kambi hii yamefungua njia kwa kambi nyingine inayotarajiwa kufanyika Januari mwakani. “Tunaomba wananchi msiogope kupima. Mkipata taarifa, jitokezeni kwa wingi. Kinga ni bora kuliko tiba,” alihimiza Bakuba.


Hamasa hiyo ilinogeshwa na ushuhuda wa Balozi wa Saratani Tanzania, Cedou Mandigo, maarufu kama “Babu wa Kitaa”. Kama shuhuda aliyepambana na saratani na kupona, Babu wa Kitaa aliwataka wananchi kuondoa hofu na imani potofu. “Mimi ni shahidi hai. Saratani inatibika ukiwahi mapema. Tusisubiri hadi ugonjwa utulemaze ndipo tukimbilie hospitali,” alieleza shuhuda huyo.


Kampeni hii ya ‘Huduma za Mkoba’ inaenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Fanya Uchunguzi — Okoa Maisha,” ikilenga kupunguza vifo vinavyotokana na saratani nchini Tanzania kwa kuhakikisha huduma zinafika vijijini ambako ndiko kuna idadi kubwa ya Watanzania.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.