Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inakabiliwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura, ambapo inapokea wastani wa wagonjwa 200 hadi 500 kila siku. Hali hii inaonesha wazi uhitaji mkubwa wa huduma hizi muhimu katika kuhakikisha maisha ya Watanzania yanaokolewa.
Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS), Dkt. Said Kilindimo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Huduma za Dharura na Ajali Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 27 Mei.
Dkt. Kilindimo alisema kuwa lengo kuu la maadhimisho haya ni kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na watoa huduma za dharura, ambao hufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maisha ya watu yanaokolewa kila siku. Alifafanua kuwa matukio yanayohitaji huduma za dharura yamekuwa yakiongezeka kwa kasi nchini kutokana na sababu mbalimbali kama vile ajali za barabarani, majanga ya asili kama vile maporomoko ya ardhi na milipuko ya magonjwa, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa janga la Uviko-19 (COVID-19) mwaka 2020/2021.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho kigumu, vitengo vya dharura vilikuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na janga hilo, kwa kuhakikisha watoa huduma na wananchi wanalindwa ipasavyo na kupata huduma stahiki.
Kwa mujibu wa Dkt. Kilindimo, tangu kuanzishwa kwa Idara ya Huduma za Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kumekuwa na mafanikio makubwa. Alibainisha kuwa vifo vya wagonjwa wanaofika hospitalini wakiwa katika hali mbaya ya dharura vimepungua kwa kiasi kikubwa cha asilimia 40. Mafanikio haya yameisukuma serikali kuongeza uwekezaji mkubwa katika eneo hili, ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali za dharura katika kila mkoa na wilaya nchini, pamoja na kuongeza vifaa tiba vya kisasa kama vile mashine za CT-Scan.
"Huduma hizi zinapatikana kwa saa 24, usiku na mchana, kutokana na juhudi kubwa za watoa huduma walio mstari wa mbele kuhakikisha kila mgonjwa anayefika anapokea matibabu yanayostahili kwa wakati," alisisitiza Dkt. Kilindimo.
Alifurahia pia kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS) kimekuwa kinara katika kuzalisha madaktari bingwa wa magonjwa ya dharura. Hadi sasa, zaidi ya madaktari 105 wamehitimu na wameanza kutoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, alikiri kuwa idadi hiyo bado haitoshelezi mahitaji halisi ya sasa kutokana na ongezeko la mahitaji.
Akizungumzia hali halisi ya huduma za dharura katika mikoa mingine nchini, Dkt. Michael Kimario, ambaye ni Daktari Mkazi na Mwanafunzi wa Udaktari Bingwa wa Magonjwa ya Tiba ya Dharura na Ajali kutoka Hospitali ya Bulongwa, Wilaya ya Makete mkoani Njombe, alieleza kuwa kuna tofauti kubwa kati ya huduma zinazotolewa Muhimbili na zile zinazopatikana katika hospitali za mikoani. Alionyesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika kuboresha huduma za dharura katika ngazi za mikoa na wilaya ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora kwa wakati wanapozihitaji.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Dkt. Julieth Magandi, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohammed Janabi, aliahidi kuwa serikali itaendelea kuweka nguvu katika kuboresha huduma za dharura ili ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati muafaka.
Takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa magonjwa ya dharura husababisha vifo vya takribani watu milioni 37.8 kila mwaka duniani kote. Takwimu za mwaka 2019 pekee zinaonesha kuwa vifo milioni 27.2 vilitokana na magonjwa ya dharura kama vile mshtuko wa moyo, ajali, na kiharusi, hivyo kuonesha umuhimu wa kuimarisha huduma hizi kwa ajili ya afya ya umma.