Katika jamii nyingi, majonzi ya kumpoteza mpendwa hubaki kuwa faragha ya familia, lakini kwa familia ya marehemu Elizabeth Michael Mushi wa Kitongoji cha Kisomboko, Uru Kusini mkoani Kilimanjaro, wamechukua hatua isiyo ya kawaida ya kubadilisha huzuni yao kuwa tumaini jipya kwa jamii. Mara tu baada ya kuvunja tanga la mama yao, familia hii imetangaza rasmi kuanzishwa kwa Taasisi ya "Elizabeth Foundation," chombo kitakachojikita katika kutoa elimu, uchunguzi na matibabu bure, kama alama ya kudumu ya kuendeleza upendo wa mama yao kwa wengine.
Dhamira kuu ya taasisi hii ni kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, hasa shinikizo la damu na matatizo ya moyo, ambayo ni tishio la kimya kimya linaloathiri maelfu ya Watanzania. Huduma hizi zitakuwa zikitolewa kila ifikapo tarehe 3 Oktoba, siku ambayo Elizabeth alifariki dunia, ikiwa ni njia ya kipekee ya kugeuza siku ya huzuni kuwa siku ya matumaini na uponyaji kwa wengine.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Mhandisi Stratton Anizety, mmoja wa watoto wa marehemu, alieleza kuwa msukumo wa kuanzisha taasisi hii unatokana na safari ya mama yao, ambaye alivumilia changamoto za kiafya kwa zaidi ya miaka 11 lakini hakuwahi kupoteza moyo wake wa kusaidia jamii. "Mama alipitia kipindi kigumu sana cha maradhi, lakini upendo wake kwa watu haukupungua. Tumeona njia bora ya kumuenzi ni kuendeleza pale alipoishia, kwa kutoa elimu na huduma za afya kwa wale wasiojiweza," alisema Mhandisi Stratton.
Mpango wa awali ni kuanza kutoa huduma katika vijiji vya Kata ya Uru Kusini na kisha kusambaa maeneo mengine nchini. Gaudens Mushi, mtoto mwingine, alisisitiza kuwa tatizo kubwa ni watu wengi kutojua hali zao za afya hadi wanapozidiwa. "Tunafuga magonjwa kimya kimya. Taasisi hii italeta utamaduni wa kupima afya mara kwa mara," alieleza.
Urithi wa Elizabeth hauishii kwenye afya pekee. Alice Cyprian Mndeme, mmoja wa wanafamilia, alifafanua kuwa taasisi hii itabeba nguzo sita alizozipenda marehemu maishani mwake: sala, upendo, elimu, afya, maendeleo, na ndoa yenye amani.
Mpango huu umepokelewa kwa mikono miwili na jamii pamoja na wataalamu. Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka KCMC, Dk. Timon Emaely, alipongeza hatua hiyo akisema ni muhimu kuwafikia wananchi vijijini na elimu ya afya. Naye Diwani mstaafu wa eneo hilo, Wakili Wilhard Kitali, ameahidi kuhakikisha usajili wa taasisi unakamilika ndani ya siku saba ili ianze kazi rasmi, huku wananchi wakionyesha furaha yao kwa matumaini ya kupata huduma zitakazopunguza makali ya maisha.