Janga la Kimya Dar: Wagonjwa Milioni 3 wa Kisukari Watishia Mfumo wa Afya, Shifaa Yaja na 'Mwarobaini' Mpya

culture | Sun Nov 16 2025


Janga la Kimya Dar: Wagonjwa Milioni 3 wa Kisukari Watishia Mfumo wa Afya, Shifaa Yaja na 'Mwarobaini' Mpya

Jiji la Dar es Salaam, ambalo ni kitovu cha biashara na hekaheka nyingi nchini Tanzania, hivi sasa limekalia "bomu" linaloweza kulipuka muda wowote katika sekta ya afya. Hali hii inatokana na takwimu za kushtusha zilizotolewa hivi karibuni zinazoonyesha kuwa idadi ya wakazi wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kisukari imepaa kwa kasi ya ajabu na kufikia watu milioni 3.


Hii ni kengele ya hatari ikizingatiwa kuwa miaka michache iliyopita, tafiti zilionyesha kuwa jiji hili lilikuwa na wagonjwa wasiozidi 600,000. Ongezeko hili la ghafla linaashiria mabadiliko makubwa ya mtindo wa maisha wa 'Bongo', ambapo ulaji usiofaa na ukosefu wa mazoezi vimeanza kutoa gharama kubwa kwa afya za wananchi.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitengo maalumu cha kisasa cha kutibu kisukari katika Hospitali ya Shifaa iliyopo jijini hapa, Mkurugenzi wa Tiba wa hospitali hiyo, Dk. Emmanuel Maganga, alifafanua kuwa hali ni mbaya na inahitaji jitihada za makusudi.


"Ukilinganisha takwimu za nyuma na sasa, utaona tunakoelekea ni kubaya. Kisukari kimekuwa janga linalokua kwa kasi ya kutisha. Kibaya zaidi, ugonjwa huu hautembei peke yake; ni chanzo kikuu cha kufeli kwa figo duniani kote. Hivyo, vita dhidi ya kisukari ni vita ya kuokoa figo za Watanzania," alisisitiza Dk. Maganga kwa masikitiko.


Mzigo Mzito kwa NHIF na Uchumi wa Mtu Mmojammoja

Athari za ugonjwa huu haziishii kwenye maumivu ya mwili tu, bali zinatafuna uchumi wa taifa. Dk. Maganga alibainisha kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unatumia kiasi kikubwa cha fedha kutibu Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs). Inakadiriwa kuwa asilimia 50 ya malipo yote ya NHIF yanaenda kwenye matibabu ya magonjwa haya, huku kisukari na figo vikiongoza orodha hiyo. Hii ina maana kuwa mabilioni ya Shilingi za Kitanzania ambayo yangeelekezwa kwenye maendeleo mengine, sasa yanatumika kupambana na matokeo ya mitindo yetu ya maisha.


Shifaa Yaja Kivingine: Huduma Jumuishi (One-Stop Center)

Ili kukabiliana na changamoto hii, Hospitali ya Shifaa imeamua kuleta mapinduzi kwa kuanzisha kitengo maalum ambacho kinatajwa kuwa ni mkombozi kwa wagonjwa. Tofauti na utaratibu uliozoeleka wa mgonjwa kuzunguka hospitali nzima kutafuta vipimo, kitengo hiki kipya kinatoa huduma zote muhimu eneo moja.


"Tumeamua kumrahisishia mwananchi maisha. Akifika hapa, ndani ya saa moja atakuwa amehudumiwa na daktari bingwa wa kisukari, amechekiwa macho na daktari bingwa (kwani kisukari huathiri macho), na amepewa ushauri na mtaalamu wa lishe. Hii ni 'package' kamili inayopatikana sehemu moja," alieleza Dk. Maganga.


Serikali na Sekta Binafsi: Ushirikiano wa Kimkakati

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Gunini Kamba, aliipongeza hatua hiyo na kusema kuwa ni uthibitisho wa nguvu ya ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP). Alisisitiza kuwa uwekezaji huo unakwenda sambamba na Dira ya Taifa ya 2050 na jitihada za kukuza utalii wa kimatibabu (Medical Tourism).


"Tanzania sasa inajielekeza kwenye utalii tiba. Tunapooona hospitali za hapa nchini zinajengwa kwa viwango vya kimataifa kama Shifaa, tunafurahi kwa sababu inapunguza ile haja ya Watanzania kwenda kutibiwa nje ya nchi, na badala yake tunavutia wageni kuja kutibiwa hapa kwetu," alisema Dk. Kamba.


Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Hospitali Binafsi (APHA), Dk. Egina Makwabe, aliongeza kuwa Hospitali ya Shifaa imeweka rekodi mpya Afrika Mashariki kwa ukubwa na ubora, jambo ambalo ni la kujivunia kwa Watanzania wote.


Rai imetolewa kwa wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kubadili mitindo ya maisha, kupunguza vyakula vya wanga na sukari nyingi, na kufanya mazoezi ili kujikinga na ongezeko hili la kutisha la magonjwa yasiyoambukiza.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.