Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasilisha kile alichokiita mafanikio makubwa ya serikali yake katika sekta ya afya, huku akitoa onyo kali kwa yeyote atakayejaribu kuvuruga amani na utulivu uliopo visiwani humo.
Akihutubia umati wa wananchi katika uwanja wa Shangani Mkokotoni, jimboni Kijini, leo Septemba 23, 2025, Dkt. Mwinyi alisisitiza kuwa amani ndio msingi wa maendeleo yote yanayoonekana Zanzibar. Alisema serikali yake itaendelea kusimamia misingi ya maridhiano, lakini haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu au kikundi kitakachochochea fujo na kuvunja amani. "Amani yetu ni jambo lisilo na mjadala. Yeyote atakayechezea amani, sheria itachukua mkondo wake bila kumuonea muhali," alisisitiza Dkt. Mwinyi.
Akigeukia mafanikio ya serikali yake, Dkt. Mwinyi alijivunia maboresho makubwa katika sekta ya afya, akisema sasa huduma zote za matibabu, kuanzia kumuona daktari hadi dawa, ni bure. Aliongeza kuwa hata wagonjwa wanaolazwa hospitalini sasa wanapatiwa chakula cha milo mitatu bila malipo yoyote.
Kwa mzaha, alisimulia jinsi maboresho hayo yalivyokuwa na mafanikio makubwa, akisema, "Huduma zimekuwa bora kiasi kwamba baadhi ya wagonjwa wakipata nafuu na kuambiwa warudi nyumbani, wanakuwa wazito kuondoka. Wanataka kuendelea kubaki hospitali kutokana na huduma nzuri wanazopata."
Pamoja na afya, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea na kasi ya ujenzi wa barabara za kisasa mijini na vijijini. Alisema miundombinu imara ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu, jambo ambalo huchochea ukuaji wa haraka wa uchumi kwa wananchi wote wa Zanzibar. Alimalizia kwa kuwaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuendelea na uongozi ili kukamilisha mipango ya maendeleo aliyoianzisha.