Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kuwa serikali zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar, zimejidhatiti katika kuendeleza mazingira rafiki na wezeshi ya kufanya biashara nchini. Aliyasema hayo jana, Julai 8, 2025, alipokuwa akifungua rasmi Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba.
Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi alitoa wito mzito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa "uzalendo wa kiuchumi" kwa kuthamini na kununua bidhaa zinazozalishwa nchini. Ili kufanikisha hili, aliziagiza mamlaka za biashara, ikiwemo Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE), kuhakikisha alama na chapa rasmi ya "Made in Tanzania" inatumika ipasavyo na kwa ufanisi ili kutambulisha na kutangaza bidhaa za ndani katika masoko ya kimataifa.
"Ni lazima tuzipende na kuzithamini bidhaa zetu. Chapa hii si kwa ajili ya masoko ya nje tu, bali inapaswa kujenga fahari na kuungwa mkono na sisi wenyewe kwanza. Tunapounga mkono vya kwetu, tunaimarisha viwanda, tunatengeneza ajira, na tunakuza uchumi," alisisitiza Rais Mwinyi.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kurahisisha mifumo ya kibiashara na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali ili kuongeza ufanisi na uwazi. Katika hatua hiyo, aliipongeza TANTRADE kwa maboresho makubwa ya miundombinu katika viwanja vya maonesho na kwa kuendesha shughuli zote za maonesho ya mwaka huu kidijitali, kuanzia usajili hadi uendeshaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Latifa Khamis, alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yamepata mwitikio mkubwa. Alitolea mfano banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, ambalo hadi kufikia jana lilikuwa limeongoza kwa kutembelewa na zaidi ya watu 190,000, wakiwemo watoto 54,000, ishara ya mafanikio na mvuto wa maonesho hayo kwa umma.