Yanga Wajilaumu, Mvuto wa Pesa za Waarabu Wamng'oa Kocha Bingwa Miloud Hamdi

sports | Fri Jul 04 2025


Yanga Wajilaumu, Mvuto wa Pesa za Waarabu Wamng'oa Kocha Bingwa Miloud Hamdi

Siku chache tu baada ya kuiongoza Yanga kutetea mataji yake mawili, Ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA, kocha Miloud Hamdi amewaacha mabingwa hao wa nchi na kutangazwa rasmi kuwa kocha mkuu wa klabu ya Ismaily ya nchini Misri. Kuondoka kwake kunatajwa kuchangiwa na Yanga kusitasita kumpa mkataba mpya huku Waarabu wakiweka mezani ofa nono.


Habari zinaeleza kuwa wakati mkataba wa miezi sita wa kocha huyo raia wa Algeria na Ufaransa ukielekea ukingoni, uongozi wa Yanga uligawanyika. Baadhi ya viongozi walitaka aongezewe mkataba mrefu baada ya kuonyesha uwezo mkubwa, huku wengine wakitaka kuendelea na mpango wa awali wa kusaka kocha mpya. Kusitasita huko kumeigharimu Yanga.


Wakati Yanga wakibishana, klabu za Ismaily (Misri), USM Alger (Algeria), na RS Berkane (Morocco) ziliingia vitani na ofa nzito, ambapo Ismaily imefanikiwa kumpata kocha huyo, ikielezwa kuwa itamlipa mshahara mara mbili ya ule aliokuwa akipokea Jangwani.


"Nadhani tulichelewa kufanya maamuzi," alisema mmoja wa viongozi wa Yanga. "Timu ilikuwa inacheza soka kubwa chini yake, mechi za mwisho zilionyesha mabadiliko ya kimbinu. Lakini alimaliza mkataba akiwa na ofa nyingine mkononi na mwisho wa siku kaamua kuondoka."


Miloud Hamdi aliletwa Yanga kama kocha wa kumalizia msimu baada ya kuondoka kwa Saed Ramovic. Alipewa mkataba mfupi wa miezi sita tu, akitokea Singida Black Stars bila kuiongoza katika mchezo wowote, huku viongozi wa Yanga wakiendelea na mchakato wa kusaka kocha mwingine. Hata hivyo, mafanikio yake yasiyotarajiwa yaliwafanya baadhi ya mabosi wafikirie upya, lakini tayari walikuwa wamechelewa.


Kuondoka kwa Hamdi sasa kunawaacha mabingwa hao wa nchi katika harakati za kuanza upya mchakato wa kutafuta kocha mwingine atakayeiongoza timu hiyo katika msimu ujao wa mashindano ya ndani na kimataifa.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.