Mabingwa wa Tanzania, Young Africans (Yanga), wanatarajiwa kuingia uwanjani kesho wakiwa na kazi moja tu akilini: kukamilisha kile walichokianza nchini Angola na kutinga hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika. Yanga itawakaribisha Wiliete Benguela katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 5:00 jioni, huku wakiwa na mtaji mnono wa ushindi wa mabao 3-0 kutoka mchezo wa kwanza.
Licha ya kuwa na faida hiyo kubwa, Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz, ameweka wazi kuwa timu yake haitaingia uwanjani kwa kuridhika. Akizungumza na wanahabari, Folz alisema wanaheshimu wapinzani wao na wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi mwingine mbele ya maelfu ya mashabiki wao watakaojitokeza kuwapa nguvu.
"Tunaongoza kwa mabao matatu, lakini katika mpira wa miguu lolote linaweza kutokea. Heshima kwa mpinzani ni muhimu. Tumejiandaa vizuri na lengo letu ni kushinda tena ili kuwapa furaha mashabiki wetu na kusonga mbele kwa kishindo," alisema Kocha Folz.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mchezaji wa timu hiyo, Aziz Andambwile, ambaye alisema wachezaji wote wapo tayari kutekeleza maagizo ya benchi la ufundi kikamilifu. "Kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza, tutafuata maelekezo ya mwalimu. Morali iko juu na tunataka kuona timu inafika mbali kwenye mashindano haya makubwa," alisema Andambwile.
Kwa upande wa wageni, Wiliete Benguela, wamekuja Tanzania wakijua wanakabiliwa na mlima mrefu wa kupanda. Kocha wao, Bruno Ferry, alikiri kuwa mchezo utakuwa mgumu mno, lakini akasisitiza kuwa timu yake haijakata tamaa na itapambana hadi dakika ya mwisho. Mchezaji wao, Mahalatsi Makudubela, aliongeza kuwa katika soka hakuna lisilowezekana na lengo lao ni kuja kupindua matokeo na kushinda.